Mwenyekiti wa Mtaa wa Chaumma apongezwa kwa ‘ubwabwa’

Mbeya. Shughuli katika Soko la Mwanjelwa jijini Mbeya zimesimama kwa muda kupisha sherehe ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Soko, Brayani Mwakalukwa, aliyeshinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa kupitia Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Katika sherehe hiyo, mamia ya wananchi wakiwamo vyama vya siasa jijini humo kama vile CCM, Chadema na CUF waliungana kwa pamoja kula ubwabwa na vinywaji kumpongeza mshindi huyo.

Mara kadhaa imekuwa ikishuhudiwa baadhi ya vyama vikijitenga pale wagombea wao wanaposhindwa katika uchaguzi, lakini imekuwa tofauti kwa mgombea wa Chaumma ambaye amejikuta akiandaliwa hafla na wananchi kumpongeza kwa ushindi wake.

Katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika juzi Novemba 27, 2024, Mwakalukwa aliibuka mshindi kwa kura 42 akiwabwaga Maria Mahinya wa CCM (kura 38) na Bahati Mwakibinga wa Chadema aliyepata kura 19.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Soko katika Kata ya Ruanda jijini Mbeya, Brayani Mwakalukwa kwa tiketi ya chama cha Chaumma.

Hata hivyo, kabla ya Mwakalukwa kujiunga na Chaumma, alitokea CCM ambayo alibwagwa kwenye kura za maoni akiachwa kwa kura tano dhidi ya Maria, licha ya kuongoza kwa kipindi kilichopita akiwa mwenyekiti.

Leo, Novemba 30, 2024, Soko la Mwanjelwa limerindima huku shughuli zikisimama baada ya wananchi, wafanyabiashara na makada mbalimbali wa vyama vya siasa, kujitokeza kusherekea ushindi wa mwenyekiti huyo.

Atupokile Hagai ambaye ni mjumbe wa CCM, amesema wameamua kumuunga mkono mwenyekiti huyo kutokana na sera zake alizoonesha kwa kipindi chote.

“Ni mtu wa watu muda mwingine hatupigi kura kuangalia chama, bali mgombea anayefaa kuongoza wananchi. Leo CCM wamenituma nikawakilishe na nimepika chakula na kula ubwabwa,” amesema Atupokile.

Naye mjumbe wa Chadema, Aida Kajuki amesema Mwakalukwa ni kiongozi mwenye sifa na hajachaguliwa bahati mbaya, bali uweledi na ushirikiano kwa wananchi.

“Anatosha sana, ametengeneza ajira binafsi kwa vijana, anachochea maendeleo katika mtaa huu, hivyo tuna sababu ya kuungana naye ndio maana tumejichanga sisi wananchi na kusherehekea ushindi wake,” amesema Aida.

Akizungumza na Mwananchi, Mwakalukwa amesema vipaumbele vyake ni afya na miundombinu,  akieleza kuwa licha ya kutofanya kampeni,  anashukuru wananchi kumrejesha katika nafasi hiyo.

Amesema akiwa mwenyekiti wa mtaa pekee nchini kupitia chama hicho, atajitahidi kuwakilisha vema ili kutowaangusha waliomuamini kumpa kura.

“Nilitoka CCM nikataka kustaafu, Chadema na ACT- Wazalendo walinifuata kila mmoja kwa muda wao nigombee upande wao, niligoma, baadaye wakaja baadhi ya wazee wakaniambia nigombee Chaumma.

“Kwa kuwa sera ya ubwabwa ni ya kila mmoja hadi mtoto mdogo, nikaona nikubali na nilitumia dakika 30 kuomba kura ambapo Novemba 26 dakika 15 zilikuwa za muziki na 15 kuomba kura,” amesema Mwakalukwa.

Mmoja wa wananchi ambaye aliungana na mamia ya wengine kusherehekea ushindi huo, Jafari Mwamwaja amesema Mwakalukwa hata angegombea peke yake bila chama chochote angeshinda kutokana na busara alizonazo.

“Hatuna wasiwasi naye katika uongozi wake, tuliona kipindi kilichopita akiwa CCM, ndio maana hii sherehe tumeiandaa sisi. Yeye hajahusika, tutaendelea kushirikiana naye,” amesema.

Related Posts