SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar leo imeahidi kuendelea kuunga mkono Mradi wa USAID Kizazi Hodari unaolenga kusaidia katika kuboresha afya, ustawi na usalama wa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu (OVC) na vijana walio katika jamii zinazokabiliwa na tatizo la VVU Zanzibar.
Kauli hiyo imetolewa leo Zanziar na Waziri wa Zanzibar Ofisi ya Rais, Mamlaka ya Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum (TAMISEMI & SD) Massoud Ali Mohammed alipokutana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Deloitte Africa Ruwayda Redfearn aliyefanya ziara Zanzibar, ziara ambayo ililenga kupata ufahamu wa jinsi ya utekelezaji wa Mradi wa USAID Kizazi Hodari pamoja Wapokeaji wa Huduma za watu wanaoishi na kupokea dawa za kufazambaza virusi vya VV (RoC).
Mradi wa USAID Kizazi Hodari Kanda ya Kusini (KHSZ) ni mradi wa miaka mitano (Machi 2022 – Machi 2027), unaofadhiliwa na Watu wa Marekani kupitia USAID na unatekelezwa na Deloitte Consulting Limited kwa kushirikiana na mashirika ya kiraia. (AZAKi).
Waziri Massoud Ali Mohammed alisema kuwa Serikali ya Zanzibar inaelewa juhudi zinazofanywa na mradi wa USAID Kizazi Hodari katika kuboresha afya, ustawi na usalama wa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi (OVC) na vijana walio katika jamii yenye matatizo makubwa ya VVU Zanzibar.
Miradi hii inakwenda mashinani na inawagusa walengwa moja kwa moja. Tunaelewa jinsi matatizo ya watoto wetu wanaoishi na VVU yanavyoenda na hasa pale ambapo wazazi wao wanapokuwa wamefariki dunia. Sisi serikali ya Zanzibar tunathamini juhudi hizo na tunaendelea kujitolea na tunatoa msaada wetu wote unaohitajika katika kufanikisha mafanikio ya mradi huu’, alisema Waziri Massoud Ali Mohammed.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Deloitte Africa Ruwayda Redfearn aliipongeza Serikali ya Zanzibar kwa msaada na ushirikiano ambao mradi wa USAID Kizazi Hodari imekuwa ikipata wakati wa kutekeleza mradi wa huu.
‘Nimefurahishwa sana na ushirikiano wa serikali ambao tumekuwa tukipata wakati wa kutekeleza mradi huu. Tumekuwa tukifanya kazi na wizara mbalimbali za serikali na kila shughuli imekuwa ikiendelea vizuri’, alisema Redfearn na kuongeza kuwa amefurahishwa na kujifunza kuhusu jukumu la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusaidia Mradi wa USAID Kizazi Hodari na mipango wa kuendeleza huduma hizo katika siku zijazo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Deloitte kwa Afrika Mashariki Anne Muraya alisema kuwa mradi wa USAID Kizazi Hodari unalenga watoto na familia kwa lengo kuu la kuboresha afya, ustawi na usalama wa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. wenye umri wa miaka 0-17 katika jumuiya zenye mizigo mikubwa pamoja na vipaumbele vinne muhimu vya huduma ambavyo ni afya, usalama, elimu na uthabiti.
Muraya aliongeza, ‘Katika mradi unaozingatia familia kama vile USAID Kizazi Hodari, wanawake wana jukumu muhimu kama watendaji wakuu katika muhtasari wa mradi na kubadilisha mazingira katika kuchangia lengo la kimataifa la 95-95-95 ambalo ni 95% ya watu wote wanaoishi na maambukizi ya VVU kupokea tiba endelevu ya kurefusha maisha, na 95% ya watu wote wanaopata tiba ya kurefusha maisha kupata ukandamizaji wa virusi ifikapo 20230’.