Azam kibaruani kuishusha Simba kileleni

IKIWA imebaki tofauti ya pointi moja kati ya Simba SC iliyoko kileleni kwa alama 28 na Azam FC iliyo nafasi ya pili na pointi 27, matajiri hao wa Chamazi wapo na kibarua cha kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Azam leo Jumapili, wanakutana na Dodoma Jiji katika Uwanja wa Jamhuri, mchezo unaotarajiwa kuwa mgumu kwa pande zote mbili. 

Licha ya Azam kuwa katika kiwango bora, rekodi zao dhidi ya Dodoma Jiji katika uwanja huo hazivutii. Katika mechi mbili za mwisho za ligi dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri, Azam walishindwa kupata ushindi. Msimu wa 2023/24 walitoka sare ya bila kufungana, huku msimu wa 2022/23 walifungwa mabao 2-1, bao pekee likifungwa na Ayoub Lyanga ambaye sasa anaichezea Singida Big Stars. 

Hadi sasa Azam imeshinda mara moja kwenye Uwanja wa Jamhuri ushindi ukiwa wa mabao 2-0 ilioupata Juni 25, 2022. Katika michezo minne kwenye uwanja huo imepata sare mbili, ushindi mmoja na kupoteza mmoja.

Ukiachana na hilo, mara mbili wachezaji  walionyeshwa kadi nyekundu, jambo linaloonyesha changamoto wanayokumbana nayo wanapocheza hapo.

Kocha wa Azam, Rachid Taoussi anajivunia kiwango bora cha timu yake ambayo imepata ushindi mfululizo katika mechi sita za mwisho za ligi.

Azam imezifunga Namungo (1-0), Tanzania Prisons (2-0), KenGold (4-1), Yanga (1-0), Kagera Sugar (1-0), na Singida BS (2-1).

Ushindi huo umewapa pointi 18, huku mechi ya mwisho kupoteza pointi ikiwa dhidi ya Mashujaa, Septemba 29, mwaka huu walipotoka suluhu. 

Dodoma Jiji kwa upande wao wanajitahidi kuimarisha hali yao baada ya kudondosha pointi nane katika mechi tano zilizopita. Wamepoteza dhidi ya Kagera Sugar (2-1), Coastal Union (2-0) na KenGold (2-2) lakini walionyesha uhai kwa kuifunga KMC 2-1 kwenye mchezo wao wa mwisho.

Kocha wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime anatarajiwa kuandaa mpango wa kuwazuia wachezaji nyota wa Azam kama Feisal Salum ambaye ameonyesha makali kwa mabao matatu na asisti nne msimu huu. 

Akizungumza kuelekea mchezo huo, kocha wa Azam, Rachid Taoussi, alisema “Dodoma Jiji ni timu ngumu hasa wanapocheza nyumbani, lakini tuna lengo moja tu kushinda na kuongoza ligi. Wachezaji wangu wapo kwenye hali nzuri, na tumejiandaa kukabiliana na changamoto yoyote.” 

Kwa upande wa Maxime alisema: “Tunawaheshimu Azam, ni timu bora na wamekuwa kwenye kiwango cha juu, lakini Jamhuri ni uwanja wetu. Tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri na kudhihirisha kuwa bado tupo kwenye ligi kwa ushindani.” 

Wachezaji wa Azam wanatarajiwa kuonyesha makali yao, wakiongozwa na Fei Toto, Iddy Seleman ‘Nado’ na Nassor Saadun. Ukuta wa Dodoma Jiji, ulioruhusu mabao 11 msimu huu, utakuwa na mtihani mgumu wa kuzuia mashambulizi ya Azam. 

Dodoma Jiji wanamtegemea mshambuliaji Wazir Jr na viungo wenye kasi akiwamo Salmin Hoza ambao waliwahi kuichezea Azam.

Simba wanasubiri matokeo ya mchezo huo kwa matarajio ya kuendelea kuongoza ligi. Mchezo huo unaibua msisimko mkubwa. Je Azam itavunja rekodi mbaya ya Uwanja wa Jamhuri na kupanda kileleni au Dodoma Jiji watakwamisha ndoto zao? Muda utaamua.

Related Posts

en English sw Swahili