Wanachopaswa kufanya maofisa Tehama taasisi za Serikali

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikijizatiti katika matumizi ya teknolojia, ikiwamo kwenye uhifadhi wa taarifa muhimu, wadau wameshauri taasisi zinazotumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliani (Tehama) kuongeza ufanisi zaidi.

Serikali tayari imeanzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi katika matumizi ya mfumo wa Tehama na imeandaa mwongozo wa matumizi bora, sahihi na salama ikiwamo ulinzi na usalama wa taarifa binafsi, mifumo vifaa na miundombinu ya Tehama.

Ushauri huo umetolewa leo Mei 8, 2024 jijini Dar es Salaam na washiriki wa warsha ya utoaji elimu iliyotolewa na waratibu wa mifumo ya Tehama Kampuni ya Dynatech Solutions ikishirikiana na Kampuni ya Oracle kutoka Marekani.

Maofisa Tehama kutoka taasisi mbalimbali wameshauriwa kutumia mfumo imara na wa kisasa utakaowezesha utendaji kazi mzuri na uhifadhi sahihi wa taarifa za kiserikali ambazo awali zilihifadhiwa kwa njia zisizo za kidijitali, zikiwamo karatasi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Dynatech Solutions, Exaud Kimboi amesema kumekuwa na changamoto kadhaa, zikiwamo upotevu wa taarifa na udukuzi.

“Ili kumaliza changamoto hizi mafunzo yanatolewa, elimu kwa watumiaji, ufahamu ili kuhakikisha teknolojia hizi zinaongeza ufanisi. Serikali inaagalia mahitaji ya teknolojia yaliyopo mbele, hivyo tunaleta suluhisho la mfumo,” amesema.

“Kuna mabadiliko ya mifumo ya Tehama tunashauri namna ya kubadili mifumo hiyo bila ya kuleta athari. Serikali inatakiwa ikae na wataalamu wake wa Tehama na binafsi wawape mahitaji yatakayokidhi wakati husika na wakati ujao,” amesema.

Amesema lazima iwepo mifumo ya kisasa yenye kukidhi mahitaji ya huduma, kwa kuwa faida yake ni kuokoa muda kwa watumiaji na hata wananchi.

Majaliwa John, Ofisa Tehama kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), amesema katika dunia ya sasa mifumo ya uhifadhi taarifa yenye usalama na uhakika ndiyo inayohitajika.

Ametoa mfano wa taasisi hiyo akisema kwa taarifa zake zinazohusu ujenzi na usanifu lazima kuwe na mfumo mzuri wa kuzitunza.

Ofisa Tehama kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Kevin Kituli amesema matarajio yake baada ya kupata ujuzi ni kufanya kazi kwa ufanisi.

“Mfano suala la ulinzi ni la muhimu kupata elimu kila wakati ili kutunza taarifa, hili ni changamoto sehemu nyingi duniani,” amesema Kituli.

Moses Mwangi, ambaye ni Meneja Uhasibu taasisi za Serikali Afrika Mashariki kutoka Kampuni ya Oracle, amesema taasisi za Serikali pamoja na binafsi zinapaswa kujiimarisha zaidi katika matumizi ya mfumo mpya na wa kisasa.

“Mfano mgonjwa akienda hospitali zaidi ya moja anapaswa taarifa zake ziwe zilezile na si anaandika mpya, kwa hiyo lazima iwepo mifumo itakayofanya kazi pamoja, kwenye taasisi mbalimbali,” amesema.

Related Posts