Simulizi ya Zuhura mwenye VVU miaka 15 katikati ya unyanyapaa  

Songea. Zuhura Juma (51), mkazi wa Mfaranyaki wilayani Songea anapozungumzia maambukuzi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), anataka jamii iwe na tafakari ya kina kuhusu yanayotokana na kujamiiana na hata njia nyingine za maambukizo.

Anasema unapofanya jambo lifikirie zaidi, mfano unamwingilia mtu bila kinga na kesho mtu huyo anatembea na mzazi wako au mwanao, inakuwaje?

Katika mahojiano na Mwananchi anasema anaishi na VVU katika mazingira ya kunyanyapaliwa, kudhalilishwa na kutengwa na jamii ikimlaumu na kumwona kwamba alijitakia kuwa na hali hiyo.

Zuhura, mama wa watoto watano, anasema ameishi na VVU kwa miaka 15 sasa na anamshukuru Mungu kwamba hakuna mtoto wake mwenye maambukizi.

Anasimulia kwamba amepitia mitihani migumu na mateso katika maisha, lakini amesimama imara kwani hajakata tamaa. Amekuwa akiwaombea na kuwaelimisha wale wanaomtendea mabaya.

Kabla ya kugundua ana VVU, anasema alikuwa akiugua homa za mara kwa mara, tena mfululizo bila kupona. Hakujua nini kilikuwa kinamsumbua. Anasema maumivu yalikuwa makali, hakuweza kulala wala kula, aliteseka.

“Nimepitia magumu, nimeteseka, nimedharauliwa na kudhalilishwa. Nilikuwa nanyoshewa vidole na majirani zangu, nasengenywa na kuzungumziwa mambo yote mabaya. Sikukata tamaa, nilipiga moyo konde na kusonga mbele maana wanangu walikubaliana na hali yangu. Sikuogopa, niliendelea kujipa tumaini na kusali nikiomba kifo chema,” anasimulia.

Kutokana na hali hiyo, anasema alikubaliana na wazo la watoto na ndugu zake waliompeleke Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea (Homso).

Huko alipatiwa ushauri kisha akapimwa, iligundulika kwamba anasumbuliwa na ugonjwa wa kifua kikuu (TB) sugu. Kama haitoshi, alipopimwa maambukizi ya VVU ilibainika kuwa ameathirika.

 “Kwa kuwa nilishapewa ushauri na nilishapitia mateso kutokana na homa zisizopona, kubanwa kifua na kikohozi kikali nilipokea majibu yangu. Nikaanza kuishi maisha mapya na maambukizi yangu ingawa awali ilikuwa kazi kubwa kukubaliana na hilo gonjwa,” anaeleza.

Anasema baada ya kubainika kwamba ana VVU, alianzishiwa dawa za kufumbaza virusi vya Ukimwi (ARV) ambazo anaendelea kuzitumia hadi leo na zinamsaidia.

Anatoa ushauri kwa watu wasiogope kupima na kujua hali za afya zao, na ambao wamebainika kuwa na maambukizi wasiache kutumia dawa, zaidi wasiwaambukize wengine kwani kufanya hivyo ni dhambi na kunaongeza idadi ya wagonjwa.

Hali ya maambukizi Ruvuma

Si Zuhura peke yake mwenye maambukizo hayo katika Mkoa wa Ruvuma. Wakati maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yakifanyika kitaifa mjini Songea leo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dk Loius Chomboko anasema kiwango cha maambukizi ya VVU katika mkoa ni asilimia 4.9 kwa takwimu za mwaka 2022/2023.

Anasema kiwango hicho kimepungua kwa asilimia 0.7 kutoka asilimia 5.6 mwaka 2017 kwa mujibu wa takwimu za Utafiti wa Viashiria vya VVU/Ukimwi na Malaria Tanzania (THMIS) wa 2016/2017.

“Kiwango hiki cha maambukizi katika mkoa bado kipo juu zaidi ya kiwango cha kitaifa ambacho ni asilimia 4.4 kwa asilimia 0.5,” anasema.

Licha ya Zuhura kusumbuliwa na unyanyapaa,  kiwango cha hali hiyo dhidi ya watu wanaoishi na maambukizi hayo ndani ya mkoa huo kimepungua kutoka asilimia 64.5 mwaka 2012 hadi asilimia 25.5 mwaka 2017, kwa mujibu wa Dk Chomboko.

Yote kwa yote, Daktari huyo anasema “kiwango cha maambukizi mapya ya VVU kimepungua kwa asilimia 28.6 kutoka watu 3,035 kwa mwaka 2017 hadi watu 2,168 kwa mwaka 2022.

“Pamoja na mafanikio haya, mkoa bado unakabiliwa na changamoto zinazodidimiza jitihada za mapambano dhidi ya VVU na utekelezaji wa malengo ya kimkakati ya kitaifa,” anasema.

Ili kuwafikia watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (Waviu), Dk Chomboko anasema wameongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma mbalimbali kwa asilimia 10 kila mwaka, ili kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2025.

Pia wamesogeza huduma karibu zaidi na wananchi katika halmashauri zote na kuyafikia malengo ya 95 tatu yaliyowekwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Ukimwi Duniani (Unaids).

Chini ya malengo hayo inataakiwa asilimia 95 ya watu wote wanaoishi na VVU kupima na kujua afya zao, asilimia 95 ya wote waliopima na kujikuta na maambukizi waanze kutumia dawa na asilimia 95 ya wanaotumia dawa wawe wamefubaza VVU).

“Katika utekelezaji wa malengo ya 95 tatu kufikia Septemba 2024, Waviu 57,421 sawa na asilimia 84.1 walikuwa wanafahamu hali zao za maambukizi, 57,160 sawa na asilimia 99.5 walikuwa wanatumia ARV na 55,445 sawa na asilimia 97.2 walikuwa wamefubaza VVU,” anasema.

Anasema kiwango cha vifo miongoni mwa Waviu wanaotumia ARV kimepungua kutoka vifo 11 kwa kila Waviu 1,000 Septemba 2020 hadi kifo kimoja kwa kila Waviu 1,000 Septemba 2024.

Akizindua maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani mwaka huu Novemba 25, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas alisema wanaoishi na VVU mkoani humo ni 68,237.

“Ndugu viongozi pamoja na wananchi halmashauri zetu zinazoongoza ni Manispaa ya Songea ikifuatiwa na Tunduru, lakini vilevile na Halmashauri ya Mbinga, hivyo napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wananchi wote kuzingatia tiba na matunzo, vilevile kuendelea kutumia dawa za kufubaza kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuendelea kupambana na matatizo haya,” alisema.

Mwakilishi wa Baraza la Watu wanaoishi na VVU na Mwenyekiti wa Shirika lisilo la kiserikali la Nacopha, Letisia Moris anasema hali ya unyanyapaa na ubaguzi ni changamoto.

“Niwaombe viongozi wa dini, viongozi wa kimila na Serikali kwa nafasi zao kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya udhalilishaji, unyanyapaa na ukatili kwa watu wanaoishi na VVU. Kwa kufanya hivi tutakuwa na jamii iliyostaarabika na yenye uelewa mkubwa wa namna ya kuheshimu haki za binadamu,” anasema.

Mkuu wa Programu wa Wizara ya Afya, Dk Catherine Joachim anasema takwimu zinaonyesha Mkoa wa Ruvuma ni kinara katika upimaji wa VVU kwa asilimia 79, huku ukifanya vema katika kutekeleza malengo ya 95 tatu.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Ruvuma inaongoza ikifuatiwa na Mkoa wa Njombe kwa asilimia 78.2 na Shinyanga kwa asilimia 78.

Malengo hayo yanaakisi asilimia 95 ya Waviu wawe wametambua hali zao, asilimia 95 wawe wamewekwa katika huduma ya tiba na asilimia 95 ya walio kwenye tiba wawe wamefanikiwa kufubaza VVU ifikapo mwaka 2025.

Dk Catherine anasema kutokana na mwamko wa upimaji, hali ya maambukizi ya VVU katika mkoa huo imepungua kwa asilimia 0.7 ukiwa mkoa unaoongoza nchini.

Katika mkoa huo, maambukizi yameshuka kutoka asilimia 5.6 mwaka 2016/17 hadi asilimia 4.9 mwaka 2022.

“Kilichojificha nyuma ya kupungua kwa maambukizi katika mkoa huu, wananchi wake wamekuwa wakipima mara kwa mara kujua afya zao,” anasema Dk Catherine.

Anasema kutokana na Mkoa wa Ruvuma kuendelea kukua kiuchumi kupitia shughuli za kilimo, migodi ya makaa ya mawe na madini mengine, usafirishaji na uvuvi maendeleo hayo yameleta nakisi kubwa kwenye usawa unaosababisha baadhi ya makundi kuwa katika hatari zaidi ya maambukizi ya VVU.

Anasema uchunguzi uliofanywa umebaini vijana wa kike kati ya miaka 15 na 24 wameendelea kuwa katika hatari hasa katika miji na vitongoji yanakopita malori ya kusafirisha makaa ya mawe, kwenye machimbo madogo-madogo na shughuli za uvuvi.

Related Posts