Nondo wa ACT-Wazalendo adaiwa kutekwa, Polisi yasema…

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Abdul Nondo anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi Luis wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam.

Nondo anadaiwa kukutwa na kadhia hiyo leo Jumapili Desemba mosi, 2024 muda mfupi baada ya kushuka katika basi akitokea mkoani Kigoma alikokuwa akishiriki shughuli za chama hasa kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Novemba 27,2024.

Mwananchi imemtafuta kwa simu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kintikwi kuzungumzia tukio hilo ambaye amesema litazungumzwa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro.

Alipotafutwa kwa nyakati tofauti, Kamanda Muliro simu zake ziliita bila kupokewa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Haki za Binadamu na Vyombo vya Uwakilishi wa Wananchi wa ACT-Wazalendo Mbarala Maharagande,  Nondo ametekwa asubuhi akitokea Kigoma alikokuwa sehemu ya viongozi wa kitaifa walioongoza kampeni kwenye mikoa ya Magharibi mwa Tanzania.

“Mashuhuda wa tukio wanasema kulikuwa na purukushani katika utekaji wa Nondo iliyosababisha begi lake ndogo kudondoka. Katibu Mwenezi wa ACT- Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala na ofisa wa harakati na matukio, Wiston Mogha waliofika mapema kituoni hapo walitambua haraka kuwa aliyetekwa ni Nondo kwa sababu walizitambua nguo zake kwenye begi lililodondoka na ‘note book’ yake,” amedai Maharagande kupitia taarifa hiyo.

Amesema ACT-Wazalendo inaendelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu tukio hilo. Machi 2018 Nondo akiwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) alidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana kisha kutekelezwa wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Related Posts