Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi imesema vifo vitokanavyo na Ukimwi, vitapunguzwa nchini, iwapo Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote itaanza kutekelezwa.
Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa maambukizi ya Ukimwi mwaka 2021 yaliua watu 25,000 na mwaka 2023 idadi hiyo ilipungua hadi vifo 22,000 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa kamati hiyo, Waviu wengi wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na magonjwa nyemelezi kwa kushindwa kulipia gharama za matibabu kutokana na changamoto za kiuchumi.
Mwaka 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alitia saini muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote na sheria kamili, baada ya kutangazwa kwenye gazeti la Serikali Desemba Mosi, 2023.
Akizungumza leo Desemba Mosi, 2024 katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ambayo kitaifa yanafanyika mjini Songea katika viwanja vya Maji Maji, Mwakilishi wa mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Christin Mzava ametaja hiyo kama suluhu ya kupunguza vifo hivyo.
“Matibabu yanatolewa bure lakini kuna magonjwa nyemelezi mtu mwingine hazuiwi kuwa nayo, bima kwa wote itawapa fursa wote waweze kuhudumiwa bila vikwazo vyovyote, itawawezesha kupima na kutibiwa magonjwa mengine bila kuwa na vikwazo vya fedha.
“Sheria hii Rais alishaisaini na tunatamani hivi karibuni itaweza kutekelezwa na watapata fursa wote na zile 95 tatu tunaomba mzidi kuongeza nguvu hasa katika suala la kupima na kutafakari ni wangapi wameathirika, katika hili wanaume wapewe kipaumbele,” amesema Dk Mzava.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Tacaids, Dk Jarome Kamwela amesema kwa kutambua rasilimali kutoka nje zinapungua, Serikali ilianza kufanya maandalizi mwaka 2015 kuanzisha mfuko wa ATF na imeendelea kutenga fedha kupitia mfuko huo.
Amesema kwa kipindi chote imekuwa ikitoa kipaumbele kuhakikisha fedha zinapatikana ili kushughulikia afua za VVU na Ukimwi.
Amesema ili kuzidi kuimarisha mfuko huo, leo utazinduliwa Mpango wa Uendelevu wa Mwitikio wa Ukimwi, unaolenga kuongoza mikakati endelevu Tanzania itakayotekeleza kufikia mafanikio mwaka 2030.
“Lengo ni kupunguza maambukizi mapya na Ukimwi kwa asilimia 95, tunataka kutoa rasilimali endelevu za ndani kufadhili shughuli za Ukimwi na ni zaidi ya fedha, kwanza ni usimamizi na uongozi na rasilimali endelevu,” amesema Dk Jarome.