Dar es Salaam. Wakati ACT-Wazalendo ikisema mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa chama hicho, Abdul Nondo ametekwa leo asubuhi, Jeshi la Polisi limesema amechukuliwa na Land Crusier nyeupe na wanafuatilia.
Nondo anadaiwa kukutwa na kadhia hiyo leo Jumapili Desemba mosi, 2024 muda mfupi baada ya kushuka katika basi kituo cha mabasi cha Magufuli jijini Dar es Salaam akitokea mkoani Kigoma alikokuwa akishiriki shughuli za chama hasa kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Novemba 27, 2024.
Msemaji wa Polisi, David Misime kupitia taarifa kwa umma amesema: “Jeshi la Polisi lingependa kujulisha kuwa, Disemba 1, 2024 majira ya saa 11.00 alfajiri katika eneo la stendi ya Magufuli Mbezi Louis Dar es Salaam kuna mtu mmoja mwanaume amekamatwa kwa nguvu na kuchukuliwa na watu waliokuwa wakitumia gari lenye usajili wa namba T 249 CMV aina ya Land Cruiser rangi nyeupe.
“Ilielezwa na mashuhuda kuwa katika purukushani za ukamataji begi dogo lilidondoshwa na baadhi ya vitu vilivyokuwemo vimetambuliwa ni vya Abdul Omary Nondo.”
Misime amesema ufuatiliaji wa tukio hilo ulianza baada ya kupokewa kwa taarifa hiyo Polisi, sambamba na kufungua jalada.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Haki za Binadamu na Vyombo vya Uwakilishi wa Wananchi wa ACT-Wazalendo Mbarala Maharagande, Nondo ametekwa asubuhi akitokea Kigoma alikokuwa sehemu ya viongozi wa kitaifa walioongoza kampeni kwenye mikoa ya Magharibi mwa Tanzania.
“Mashuhuda wa tukio wanasema kulikuwa na purukushani katika utekaji wa Nondo iliyosababisha begi lake ndogo kudondoka. Katibu Mwenezi wa ACT- Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala na ofisa wa harakati na matukio, Wiston Mogha waliofika mapema kituoni hapo walitambua haraka kuwa aliyetekwa ni Nondo kwa sababu walizitambua nguo zake kwenye begi lililodondoka na ‘note book’ yake,” amedai Maharagande kupitia taarifa hiyo.