Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango ametoa wito kwa wanachama wa CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) kuvumbua njia zinazotekelezeka katika kuhamisha teknolojia zitakazowasaidia vijana ambao idadi kubwa ya Watanzania kwa sasa.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Mpango ametoa kauli hiyo Jumamosi, Novemba 30, 2024 alipomwakilisha Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika sherehe ya kufunga mwaka ya CEOrt iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema ni muhimu kuwasaidia vijana katika teknolojia za kijani, kuunga mkono tafiti na maendeleo pamoja na kuanzisha vituo atamizi vya teknolojia. Amewasihi kupitia upya vigezo vya kujiunga na CEOrt ili kuongeza idadi ya vijana kutoka biashara zinazochipukia kama masuala ya burudani, Tehama na michezo.
Aidha, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) kahamasisha wanachama waokuipa kipaumbele ajenda ya mabadiliko ya tabianchi.
Amewasihi kuongeza jitihada katika ushirikiano na suluhu za kibunifu ambazo zitahusianisha shughuli za taasisi zao na malengo ya Taifa ya uhifadhi wa mazingira pamoja na kutumia fursa zinazotokana na uhifadhi.
Vilevile, Dk Mpango amesema unahitajika ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi katika kutafuta mwelekeo sahihi kuelekea uchumi wa kijani ambao unaunga mkono maendeleo endelevu na kuendana na vipaumbele vya Taifa.
Pia, amesema wakati Serikali inaendelea kuchukua hatua kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana, ikiwemo kubadili mitalaa itakayowezesha kuendana na soko la ajira, CEOrt inapaswa kuongeza wigo wa shughuli zake ili kuongeza ajira zaidi, kutoa mafunzo kwa vitendo na mitaji kwa biashara zinazochipukia kwa wahitimu.
Amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini, ikiwemo mabadiliko ya sera na miundo ya kitaasisi ili kudhibiti urasimu pamoja na rushwa, hivyo kuchagiza sekta binafsi shindani.
Makamu wa Rais amesema Serikali imeimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuhamasisha diplomasia ya uchumi, ili kulifanya Taifa kuwa kiungo muhimu kikanda na kimataifa pamoja na kuvutia uwekezaji kutoka mataifa ya nje.
Ametoa wito wa kuongeza ushirikiano wa kibunifu baina sekta binafsi na Serikali katika kuchochea mageuzi ya kiuchumi na kijamii nchini.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, Santina Benson amesema jukwaa hilo linajivunia hatua za maendeleo, ikiwemo kuitisha majukwaa ya kujadili maendeleo ya kiuchumi kupitia sekta za viwanda na biashara.
“Miaka hii imekuwa ya mabadiliko makubwa kwa CEO Roundtable, kwani tumepiga hatua kubwa katika maeneo yetu muhimu ya kipaumbele na kuendelea kutumia jukwaa kuanzisha mijadala ya masuala muhimu kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi ya nchi,” amesema Benson.
Amesema CEOrt imeendelea kufanya juhudi za kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali kama nishati, mipango ya urithi wa biashara za familia, maendeleo ya rasilimali watu, fursa za usafirishaji na umuhimu wa uchambuzi wa data katika kukuza maendeleo ya Tanzania.