Banda ashinda kesi ya mamilioni

SHIRIKISHO la Soka duniani (Fifa) limeiamuru Richard Bays FC aliyokuwa akiichezea Abdi Banda kumlipa nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania pesa zake za mshahara na usajili anazowadai.

Msimamizi wa beki huyo wa zamani wa Simba, Fadhili Omary Sizya alisema ni kweli FIFA imeiagiza Bays kumlipa Banda Sh115,911,440, baada ya kushinda kesi ya madai aliyoifungua mwezi uliopita.

“Ameshinda kesi na klabu imepewa siku 45, bado pesa hazijalipwa kwa Banda na kwa sasa hawezi kusema chocote lakini ni kweli,” alisema Sizya.

Kama klabu hiyo haitamlipa Mtanzania huyo ndani ya muda huo itakutana na rungu la kufungiwa kusajili wachezaji wapya wa ndani na wa kimataifa kwa misimu mitatu.

Nyota huyo aliichezea timu hiyo msimu uliopita kabla ya kurejea Baroka FC ambako hakupata nafasi kubwa ya kucheza kwani katika msimu huo alicheza mechi nane za mashindano yote.

Banda aliwasilisha malalamiko kwa chombo cha kusimamia malalamiko ya mikataba kwa wachezaji (Dispute Resolution Chamber, DRC) Novemba 21 mwaka huu dhidi ya klabu hiyo kwa madai ya kuvunjiwa mkataba wake.

Hatua ya Banda ya kufikisha suala hilo FIFA ilikuja baada ya changamoto alizokutana nazo akiwa klabuni ikiwemo kutolipwa mishahara na ukosefu wa nafasi za kutosha za kucheza.

Hii sio mara ya kwanza kwa Banda mwenye umri wa miaka 29, kukumbana na kesi hiyo, kwani mwaka 2023 akiwa na Chippa United ya Afrika Kusini alifungua kesi ya madai baada ya timu hiyo kuvunja mkataba wake mapema mwaka mmoja tu baada ya kujiunga.

Chipa ilishindwa kumlipa Mtanzania huyo kwa muda uliopangwa kiasi cha Sh180 milioni jambo lililoifanya klabu hiyo kupigwa rungu la kusajili wachezaji kabla ya baadae kumalizana naye na Januari ikaondolewa adhabu hiyo.

Related Posts