Serikali kuondoa mikondo miwili shuleni Zanzibar

Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema inaendelea kuweka kipaumbele katika sekta ya elimu kujenga madarasa mengi kuondoa mikondo miwili shuleni.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,  Hemed Suleiman Abdulla amesema hayo leo Jumapili Desemba mosi, 2024 wakati akiweka jiwe la msingi  kwenye shule nne za sekondari kwa mpigo Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema hatua hiyo ni muhimu ya kuweka mazingira bora katika kujifunza na kufundishia.

“Ujenzi wa shule hizo una lengo la kuleta ufanisi na utendaji kazi katika sekta ya elimu ikiwamo kuwawezesha wanafunzi wote wa Zanzibar, kuingia kwa mkondo mmoja wa asubuhi pekee jambo litakalosaidia kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi hao,” amesema Hemed.

Akifafanua hilo, Hemed amesema Serikali imedhamiria kuimarisha miundonbinu ya elimu ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira rafiki wakiwa na nyenzo zote muhimu.

Makamu wa Pili wa Rais amesema Rais Hussein Mwinyi amefanya kazi kubwa ya ujenzi wa miradi ya maendeleo kuelekea shamrashamra za Sherehe za Mapinduzi mwaka huu na kwamba, zaidi ya miradi 150 itafunguliwa ambayo itasukuma zaidi kasi ya maendeleo nchini.

Kutokana na hilo, amewataka wananchi kuwa tayari kupisha ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa masilahi ya Taifa huku akiwahakikishia kuwa, kila atakayetoa eneo lake kupisha miradi ya maendeleo atapatiwa stahiki yake kwa mujibu wa taratibu na sheria.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa amesema miradi ya elimu imegusa maeneo yote ya Zanzibar ikijumuisha ujenzi wa shule za ghorofa, shule za chini, ujenzi wa madarasa mapya na ukarabati wa madarasa yaliyochakaa pamoja na  kuboresha miundombinu ya vifaa vya kusomea na kufundishia.

Amesema Serikali imepanga kuongeza bajeti ya elimu itakayotumika kuendeleza miundombinu ya elimu na kukuza ubora wake Zanzibar.  

Akisoma taarifa ya kitaaluma Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdulla Said amesema shule hizo nne zitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 6,000 kwa wakati mmoja kwa uwiano wa wanafunzi 45 kwa kila darasa.

Khamis amesema ujenzi wa shule hizo na nyingine zinazoendelea kujengwa Unguja na Pemba zina lengo la kupunguza changamoto ya msongamano wa wanafunzi darasani na kuakisi dhamira njema ya Serikali.

Shule hizo za ghorofa zitagharimu zaidi ya Sh30 bilioni zinazotarajiwa kufunguliwa Januari mwaka 2025.

Related Posts