MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga Princess, Mary Mbewe amejiunga na ZESCO Ndola Girls inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Zambia.
Mbewe ambaye aliachana na Yanga msimu uliopita baada ya mkataba wake wa miezi sita kumalizika, ametua klabuni hapo kama mchezaji huru akiwa pia anaitumikia timu ya taifa ya Zambia.
Nyota huyo akiwa nahodha wa kikosi hicho za taifa chini ya miaka 20 ‘Young Queens’, alikiongoza kutwaa ubingwa wa COSAFA wikiendi iliyopita.
Mbewe aliyesajiliwa Yanga Princess msimu uliopita, aliondoka akiwa hajagusa nyavu za timu yeyote iliyoshiriki ligi hiyo katika mechi 18.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa mchezaji huyo, Charles Haalubono ambaye pia aliwahi kuifundisha Yanga, alisema;
“Wakati naondoka Yanga nilitimka naye baada ya mkataba wake kumalizika kwa hiyo akarejea Zesco ambako aliwahi kucheza hapo mwanzo na sasa yuko anaendelea na majukumu ya Taifa,” alisema Haalubono.
Licha ya kocha huyo kutotaja sababu ya kuondoka kwa nyota huyo, lakini Mwanaspoti linafahamu Mbewe hakuwa chaguo la Edna Lema ambaye kwenye masharti ya mkataba wake alitaka kusajiliwa nyota wapya.