Othman azifariji familia zilizoathiriwa na upepo Pemba

Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud amezitembelea na kuzifariji familia 28 zilizoathiriwa na upepo Wilaya ya Micheweni Kaskazini Pemba.

Upepo huo ulioambatana na mvua ulitokea Oktoba 22, 2024 katika Shehia ya Mgogoni kisiwani hapo na kuziacha baadhi ya kaya bila makazi. 

Akiwa katika familia hizo Desemba mosi, 2024 Othman amesema kuzuka kwa upepo mkali, vimbunga, matetemeko ya ardhi na mvua zisizotabirika katika maeneo mbalimbali duniani ikiwamo Zanzibar ni  miongoni mwa athari zinazotokana suala la mabadiliko ya tabianchi. 

Miongoni mwa athari zilizosababishwa na upepo huo ni  nyumba zipatazo 14 kuharibika, baadhi kupeperuka mabati, kuharibika kwa mazao ya chakula na biashara, kuanguka miti mikubwa na kuathiri baadhi ya nyumba zilizokuwa karibu na miti hiyo.

Othman amewafahamisha wananchi hao kwamba Serikali itaendelea kuwa pamoja nao, kusaidia jitihada za pamoja katika kuhakikisha maisha yao yanarudi katika hali ya kawaida.

“Mamlaka zinazohusika na usimamizi wa masuala ya maafa zinaendelea na kazi ya kufanya tathmini ya madhara yaliyotokana na upepo huo ili kuhakikisha kunapatikana taarifa sahihi za kiwango cha madhara hayo na kuweza kuchukua hatua zinazostahiki kwa mujibu wa sheria ya kusimamia masuala ya maafa  hapa Zanzibar,” amesema. 

Amesema katika baadhi ya nchi mbalimbali duniani zenye visiwa kama Zanzibar kwa kijiografia, zimekuwa zikikumbana na maafa ya aina hiyo takribani kila mwaka zaidi ya mara moja au mbili.

Ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuendelea kumshukuru Mungu hasa kwa kuwa, Zanzibar kijiografia haipo katika eneo hatarishi kama zilivyo nchi nyingine duniani. 

Pamoja na kuwapa kifuta machozi (kiasi cha fedha ambacho hakikutajwa), Othman amezifariji familia hizo na kuahidi kuwa atakuwa balozi kuhakikisha wananchi hao wanapatiwa misaada.

wa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib amesema tayari Serikali ya Mkoa imeanza kuchukua hatua za awali kuwasaidia wananchi hao wakati ikendelea kusubiri tathmini kamili ya athari za maafa hayo ikamilike na hatua zaidi stahiki ziweze kuchukuliwa na Serikali. 

Mkurugenzi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Makame Khatib Makame amesema Serikali kupitia ofisi hiyo inaendelea kufanya tathmini rasmi ili kupata taarifa kamili na sahihi na kutambua kiwango cha athari zilizotokana na maafa hayo.

Amesema upepo huo uliozuka saa 4:00 asubuhi ulikuwa mkali na athari  kwa wananchi hao pia ilikuwa kubwa kwa kuwa nyumba na vibanda vya biashara viliharibiwa.

Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harous Said Suleiman amewataka wananchi hao kuwa wastahamilivu na kuendelea kuonesha upendo na umoja miongoni mwao kwa kusaidiana kwa kuwa kutokea kwa maafa hayo kunatokana na uwezo wa Mungu.

Baadhi ya waathirika hao licha ya kushukuru kwa kutembelewa na viogozi, wameomba waendelee kusaidiwa kwa kuwa wamepata madhara ya kuharibiwa mali zao.

Related Posts