KOCHA wa Alliance Girls, Ezekiel Chobanka inaelezwa yuko mbinoni kujiunga na Ceasiaa Queens ya Iringa kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Kocha huyo ameifundisha Alliance kwa zaidi ya misimu 15 akiwatengeneza baadhi ya nyota wa kike wanaokipiga nje akiwemo Aisha Masaka wa Brighton, Enekia Lunyamila (Mazaltan, Mexico) na Aisha Mnunka wa Simba Queens aliyeibuka mfungaji bora msimu uliopita akiweka kambani mabao 20.
Ndani ya misimu hiyo aliyofundisha Alliance aliwahi kupita Tiger Queens iliyoshuka daraja mwaka 2023 akisimamia mechi tatu na kurejea tena Mwanza.
Mmoja wa viongozi wa Ceasiaa (jina tunalo) alisema hawakuanza msimu na kocha mpya baada ya Noah Kanyanga kutimka kikosini hapo na walikuwa wanawatumia makocha wa muda.
“Malengo ya timu ni kumaliza tatu bora lakini hadi sasa hatujawa na matokeo mazuri tangu msimu uanze, matamanio ya viongozi ni kumpata Chobanka ambaye ana uzoefu wa ligi na anajua kuwatumia vijana wadogo,” alisema kiongozi huyo.
Mwanaspoti ilipomtafuta Chobanka juu ya ishu hiyo alisema “Mambo yakienda sawa nitakueleza lakini kwa sasa siyo muda mzuri wa kuzungumzia.”