Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) Gilead Teri amesema huenda mwaka huu Tanzania ikavunja rekodi ya kujasili miradi mingi ya uwekezaji iliyodumu kwa miaka 11.
Teri alisema hadi Novemba 29, 2024 TIC ilikuwa imesajili jumla ya miradi 800, idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni lakini pungufu ya rekodi iliyowekwa mwaka 2013 ambapo kituo kilisajili miradi 865.
Kiongozi huyo mwenye dhamana ya kuvutia na kusajili miradi nchini alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 20 ya kampuni ya vinywaji ya Mega Beverages iliyoenda sambamba na kutambulishwa kwa toleo maalumu la bidhaa yake ya K-Vant.
“Mwaka huu utakuwa mwaka wa rekodi, tangu mwaka 1997 tulipoanza kusajili rasmi miradi mwaka 2013 ndiyo unaoshikiria rekodi lakini sasa kuna uwezekano mkubwa wa kuivunja kutokana na ongezeko kubwa la miradi mwaka huu,” alisema Teri.
Teri aliongeza kuwa jambo zuri ni zaidi ni kuwa kati ya miradi iliyokuwa imesajili hadi Novemba 29, 260 ni ya wazawa na zaidi ya nusu ya miradi yote ina ushiriki wa Wazawa.
Teri alisema katika miradi iliyosajiliwa mingi ni ya uzalishaji wa bidhaa za mahitaji ya kila siku, sekta ya ujenzi, majengo, uchukuzi, kilimo na utalii.
Alisema mafanikio hayo ni matokeo ya mageuzi yaliyofanywa katika kuvutia uwekezaji kwa kubadilisha mazingira huku akisema kuwa yako thabiti na yanavutia kuliko wakati wowote ule katika nchi.
“Mbali na mazingira ya kisera yanayovutia pia Tanzania ina rasilimali nyingi, nishati ya uhakika, soko kubwa na nguvu kazi ya kutosha kufanya uzalishaji wenye tija na kumfanya mwekezaji kukua na kupata faida,” alisema.
Akizungumzia kuhusu miaka 20 ya Mega Teri alisema ni mafanikio makubwa kwani sekta waliyopo ni ngumu na ina ushindani mkubwa.
Hali ya sekta ya vinywaji
Katika hafla hiyo ambayo ilihudhuria na wadau mbalimbali, wafanyakazi wa Mega na baadhi ya wateja wao Teri alisema kusimama kwa kampuni hiyo ni ishara kuwa wazawa wanaweza.
“Mauzo ya sekta ya viwanjwa kwa mwaka 2023 yalifikia Dola za Marekani 3 bilioni (Sh8 trilioni), kati ya kiwango hicho vinywaji vikali vilikuwa na thamani ya mauzo ya Dola 721 milioni (1.8 trilioni),” alisema Teri.
Aidha Teri alisema kati ya vinywaji vyote vya Sh8 trilioni vilivyouzwa hapa nchini katika mwaka huo asilimia 80 hadi 90 vilikuwa vimezalishwa hapa nchini hususani bia.
“Tuna Imani kuwa ndani ya miaka miwili ijayo hiyo asilimia ya vinavyozalishwa nje ya nchi nayo itapungua au kumaliza kabisa na wazalishaji wa ndani. Tunavutia uwekezaji wa wanaozalishaji nje ya nchi waje zalishe hapa,” alisema.
Awali akizungumza katika hafla hiyo Meneja wa Chapa ya K-Vant Awatif Bushiri alisema mpaka sasa kinywaji chao kinauzwa katika mataifa manne nje ya nchi, ambayo ni Kenya, Rwanda, Congo DRC na Malawi.
Kuhusu toleo maalumu la chapa yake Bushiri alisema ni mahususi kwa ajili ya zawadi msimu huu wa sikukuu ndiyo maana imewekwa kwenye mwonekano wa kipekee huku ikipewa radha mpya na rangi ya dhahabu.
“Kwa kawaida spirit huwa haiwekwi kwenye maleo yam bao lakini hii imeweka, imepikwa kwa miezi mitatu ndiyo maana ina radhi ya dhahabu na radha ya kipekee,” alisema na kuongeza kuwa sasa itapatikana maduka hadi mapema mwaka 2025.