MSHAMBULIAJI wa Ain Diab ya Morocco, Jaruph Juma amesema anatamani kuendelea kufanya vizuri kwenye ligi hiyo kubwa baada ya kufunga hat-trick ya kwanza ikiwa siku chache tu tangu aliposajiliwa.
Timu hiyo ilipata ushindi wa mabao 5-0 kwenye mchezo wa Ligi kuu ya Soka la Ufukweni ya Morocco (Beach Soccer) dhidi ya Hercules huku Jaruph akifunga mabao matatu katika mchezo huo.
Akizungumza na Nje ya Bongo, Jaruph alisema haikuwa rahisi kufunga mabao hayo kwenye mchezo wake wa kwanza tangu atambulishwe na yanamfanya aendelee kupambana.
Jaruph aliongeza, amekuwa akiwafunga Morocco hasa wanapokutana kwenye mashindano ya timu za taifa hivyo ni kama mwendelezo tu wa kile anachokifanya.
“Nashukuru kwanza kwa kusajiliwa na klabu kubwa na sio rahisi nchi kama Morocco iliyoendelea kwenye soka la ufukweni na michezo mingine kukiwasha halafu ukiwa Mtanzania hilo ni jambo la kipekee,” alisema Jaruph.
Mshambuliaji huyo anakuwa Mtanzania wa kwanza kwenye soka la ufukweni kusajiliwa nje ya nchi (Morocco) na kuandika historia kwenye mchezo huo.
“Ni kweli kwanza nafurahia kuandika historia hiyo, pia naamini kucheza Morocco inatakuwa njia kwa wachezaji wengine kutimiza ndoto yao ya kucheza nje,” alisema na kuongeza;
“Nimekuwa nikiwafunga Morocco kila tunapokutana kwa hiyo haikuwa ugumu mimi kunisajili kutokana wananiona mara nyingi kwenye majukumu ya taifa.”
Jaruph aliwahi kukipiga soka la kawaida akiitumikia Simba (2016), Yanga U-20 (2015), African Lyons kwa misimu mitatu kuanzia mwaka 2019 hadi 2021.