INEC yatoa neno kwa mawakala wa vyama vya siasa

Moshi. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuwa, ingawa mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, hawatakuwa na mamlaka ya kuingilia utendaji wa watendaji wa tume.

Hayo yameelezwa leo Jumapili Desemba mosi, 2024 na Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru  ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji mstaafu Mbarouk  Mbarouk wakati wa  mafunzo kwa Mratibu wa uandikishaji wa Mkoa, maofisa waandikishaji na  wasaidizi ngazi ya jimbo, maofisa uchaguzi, ugavi na Tehama wa halmahauri mkoani Kilimanjaro.

Mbarouk amesema kazi kubwa ya mawakala wa vyama vya siasa, itakuwa ni kuwatambua waombaji wa eneo husika ili kuweka uwazi katika shughuli hiyo na kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima.

“Wakati wa uboreshaji wa daftari, mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapigakura, jambo hili ni muhimu kwani litasaidia kuleta uwazi, lakini mawakala hao hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni,” amesema Mbarouk.

Aidha, amewataka maofisa uandikishaji kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa umakini ikiwamo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji vinavyotarajiwa kutumika katika maeneo mengi , kwa kuwa Serikali imetumia gharama kubwa katika ununuzi wake.

“Lakini pia hakikisheni mnatoa ushirikiano kwa asasi zilizopewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uboreshaji wa daftari hilo, kwa Mkoa wa Kilimanjaro unatarajia kuanza Desemba 11 hadi 17 , 2024, kwani matokeo chanya na bora ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura yanategemea uwepo wa ushirikiano mkubwa kati ya wadau wote wa uchaguzi,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi, ofisa uandikishaji  Jimbo la Moshi Vijijini, Horise Kolimba amesema mafunzo wanayopatiwa yatawajengea uwezo ili kuwezesha wananchi kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na kupata fursa ya kushiriki uchaguzi mkuu mwakani.

Mwalimu Rajabu Yateri ambaye ni ofisa uandikishaji Wilaya ya Hai, amesema mafunzo hayo yana tija kubwa kwao katika kufanikisha shughuli ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapugakura mkoani Kilimanjaro.

Related Posts