Ambokile aanika mikakati mipya Mbeya City

MSHAMBULIAJI wa Mbeya City, Eliud Ambokile amesema msimu huu kuna uwezekano mkubwa wa kukipigania kikosi hicho ili msimu ujao kirejee tena Ligi Kuu Bara, kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina yao wachezaji, wadau na viongozi kiujumla.

Nyota huyo aliyefunga mabao manne ya Ligi ya Championship alisema msimu huu mwitikio kwao ni mkubwa tofauti na msimu uliopita, huku akieleza wadau kutoka jijini Mbeya wanajitolea ili kufanikisha malengo hayo.

“Sapoti ni kubwa sana kuanzia kwetu sisi wachezaji wenyewe na viongozi kiujumla, sitaki kuweka ahadi ya kufunga mabao mangapi msimu huu, ila jambo ninalolipambania ni kuhakikisha Mbeya City inacheza Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao,” alisema.

Ambokile aliyeichezea Mbeya City tangu 2017, amewahi kucheza timu mbalimbali zikiwemo za, Black Leopards FC ya Afrika Kusini kisha kurejea tena hapa nchini ili kukitumikia kikosi hicho na baadaye kujiunga na TP Mazembe kutokea DR Congo.

Kwa sasa ni msimu wake wa tatu kuichezea timu hiyo tangu aliporejea nchini akitokea Zambia alikokuwa anaichezea Nkana FC, huku akikabiliwa na deni kubwa la kukirejesha kikosi hicho Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023.

Related Posts