Wanaume watakiwa kuwashika mkono wake zao wenye maono

Dar es Salaam. Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Mhandisi Zena Said amewataka wanaume kwenye maeneo mbalimbali kuwapa ushirikiano wake zao haswa wenye maono makubwa ya kiuchumi na kijamii.

Ametoa kauli hiyo kwenye hafla ya utoaji tuzo za Malkia wa Nguvu zinazoendeshwa na Clouds Media Group zilizofanyika mwishoni mwa wiki huku malkia tisa wakipewa tuzo hizo kwenye sekta mbalimbali wanazohudumia.

Amesema wanaume wakiwapa ushirikiano wake zao itawajengea kujiamini ambapo watatimiza ndoto zao jambo ambalo litawainua kiuchumi.

Katika hafla hiyo miongoni mwa washindi waliotangazwa ni pamoja na Ramla Juma mkazi wa Pemba, aliyeshinda kipengele cha biashara ya chakula. 

Ramla ambaye kwa sasa ni mpishi mkubwa aliyeanza kupika akiwa mtaani mpaka baadae kuajiriwa Ikulu kama mpishi, lakini bado alikua na ndoto ya kusimamisha biashara yake mwenyewe, kwa sasa amefanikiwa kusimamisha biashara yake na ameajiri zaidi ya wafanyakazi 200.

Mwingine ni Aisha Mohamed (Hijab Dj) aliyeshinda tuzo ya Sekta ya Burudani, akiwa Binti mdogo aliyezua gumzo kwa kuonekana DJ anayepiga muziki bila kuonyesha maungo yake huku akivaa hijab.

Mshindi Mwingine ni Saida Mohamed, aliyeshinda tuzo ya Sekta ya viwanda kupitia biashara ya viungo mbalimbali vya chakula, ameifanya kazi hii kwa miaka kumi sasa.

Sekta ya ujasiriamali bora tuzo imeenda kwa watu wawili, huku wa kwanza akiwa Fatma Masimba aliyeanza kuwa mhudumu wa maapokezi wa hotel baadae akawa mmiliki mwakilishi, kwa sasa yeye ni mkurugenzi katika biashara kubwa ya familia yake.

Ujasiriamali tuzo nyingine imeenda kwa Fatma Abdalah (Bi Sufa), ambaye awali aliozeshwa akiwa na miaka 14 mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi, baadae matokeo yalitoka akawa amefaulu hivyo akaendelea na masomo.

Alipomaliza shule, alianza maisha yake ya ujasiriamali na bishara nyingi katikati ya changamoto. kutokana na maisha yake kutopata msingi mzuri wa kusoma aliamua kuanzisha shule na kuziita Sufa Schools ambazo zipo kwa zaidi ya miongo miwili.

Aidha, tuzo sekta ya ustawi wa jamii imeenda kwa Wanu Ameir ambaye ni mwanzilishi wa Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation, kupitia taasisi hiyo imeboresha huduma za afya ya uzazi na akili sambamba na kutoa mafunzo muhimu kwa wahudumu wa afya wa jamii.

Katika sekta ya mitindo na urembo mshindi ni Tatu Suleiman, aliyeamua kuongeza thamani ya zao la mwani kwa kutengeneza vipodozi asili.

Aida katika sekta ya utalii, Mafunda Faki ndiye mshindi ambae ni mwanzilishi na mkurugenzi wa ZanVacay iliiyomtambulisha katika ulimwengu wa kukutana na vijana, kutoa mafunzo mbalimbali yanayohusisha uongezaji wa thamani.

Tuzo ya Heshima imeenda kwa Mama Mariam, Mke wa Rais wa Zanzibar, muanzilishi wa taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) iliyowagusa wanawake wanaojishughulisha na uchumi wa buluu kwa makundi na kuwapatia boti za kisasa zenye mashine, vifaa vya kazi, na tumaini jipya na kubadilisha taswira ya maosha yao.

Related Posts