Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Uthibiti Ubora wa Shule kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mwalimu Ephrahim Simbeye amesema mafunzo hayo yataleta mabadiliko makubwa kutokana na watoa mada wabobezi walioandaliwa kwa ajili ya mafunzo hayo.
Aidha amewasihi Wathibiti Ubora kuwasikiliza kwa umakini watoa mada ili elimu hiyo iwasaidie na wengine waliobaki ofisini kwa lengo la kuboresha kiwango cha elimu na kuingia katika mashindano ya Kikanda na Kidunia.
Vilevile amewataka kuthibiti ubora wa ndani ya shule, kushirikisha jamii katika masuala ya maendeleo ya elimu, kusimamia unasihi na ushauri nasaha kama ilivyo katika suala la maadili.
“Nawakumbusha kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo hapa Mkoa wa Arusha ili kuliingizia Taifa mapato, hii inawezekana kukifanyika utaratibu mzuri ili mkafurahie mandhari na utajiri uliopo katika vivutio hivyo” ameongeza Simbeye.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Ualimu Huruma Mageni amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kutokana na umuhimu wa elimu ya amali iayolenga kuleta chachu na matokeo makubwa katika teknonojia na kujitegemea.
Pia Mthibiti Ubora Elimu wa Halmashauri ya Wilaya Newala Mkoani Mtwara Rashid Rashid amesema wawezeshaji wameanza kutoa mwanga na maelekezo kuhakikisha elimu y amali inaboreshwa.
“Kwa upande wangu changamoto ninazoziona ni upungufu wa walimu katika shule za amali, vifaa vya kufundishia na miundombinu michache kwa maana ya maktaba na maabara” ameeleza Rashid.