Sh2.9 bilioni kutumika kukarabati Chuo cha Maofisa Tabibu Simiyu

Simiyu.  Serikali kupitia Wizara ya Afya imetangaza kutoa Sh2.9 bilioni kwa ajili ya kukarabati na kujenga upya Chuo cha Maofisa Tabibu Maswa, kilichopo mkoani Simiyu.

Chuo hicho kimehudumu kwa zaidi ya miaka 50 huku hatua iliyopo ni kuboresha miundombinu na mazingira ya kujifunzia kutokana na uchakavu wa majengo ya chuo hicho.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema hayo leo Jumapili Desemba mosi, 2024 katika mahafali ya 48 ya chuo hicho yaliyofanyika mjini Maswa.

Amesema chuo hicho kimechangia kuzalisha maofisa tabibu wanaotoa huduma muhimu za afya nchini, hivyo Serikali imeamua kukiboresha kwa kujenga miundombinu ya kisasa.

“Niwahakikishie kuwa, kufikia Juni, 2025, changamoto za upungufu wa vyumba vya madarasa, maabara, mabweni na vifaa vya kufundishia zitakuwa zimetatuliwa,” amesema Dk Mollel.

Amesema tayari Serikali imeshatoa Sh2.9 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho na fedha zingine zaidi zitatolewa mwakani ili kukamilisha maboresho hayo.

Chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1974, kilianza kwa kutoa mafunzo ya cheti kwa Waganga Wasaidizi Vijijini na sasa kinatoa Stashahada ya Utabibu.

Mkuu wa chuo hicho, Dk Hangwa Hangwa amesema tangu kuanzishwa kwake, chuo hicho kimezalisha wataalamu 2,255 na kina eneo la hekta 6.11 linalofaa kwa maendeleo zaidi ya miundombinu.

Hata hivyo, Rais wa Serikali ya Wanachuo, Simba Gulala ameainisha changamoto za uchakavu wa majengo na upungufu wa vifaa vya kufundishia, hali inayokwamisha juhudi za kujifunza katika mazingira bora.

Wazazi na viongozi waliopokea tangazo hilo kwa shukrani wamesisitiza kuwa, uboreshaji wa chuo hicho utaimarisha uzalishaji wa wataalamu wa afya na kuimarisha huduma za afya nchini. Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amesema hatua hii inaakisi dhamira ya Serikali ya kuwekeza katika sekta ya afya kupitia elimu bora na miundombinu ya kisasa.

Jumla ya wahitimu 85 wa stashahada ya utabibu wametunukiwa vyeti katika mahafali hayo.

Related Posts