Dar es Salaam. Benki za Equity Tanzania Limited (EBT) na Equity Kenya Limited (EBK) zimeshinda kesi nyingine ya mgogoro wa mkopo wa Dola 47.22 milioni za Marekani (zaidi ya Sh125 bilioni), ikiwa ni kesi ya saba za namna hiyo kushinda kwa mwaka huu pekee.
Kesi hiyo ilikuwa imefunguliwa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara na kampuni za Kahama Oil Mills Limited na Kahama Oil Mills na Kahama Import & Export Commercial Agency Limited na wenzao wengine dhidi ya benki hizo, EBT na EBK.
Katika kesi hiyo ya kibiashara namba 78/2023, kampuni hizo zilikuwa zikipinga kudaiwa na benki hizo zikidai benki hizo hazikuzikopesha kiasi chochote cha pesa.
Benki hizo zilizowakilishwa na wakili Sinare Zaharan kutoka Kampuni ya Uwakili ya Rex Attorneys nazo zilifungua madai kinzani dhidi ya kampuni hizo.
Katika madai hayo, zilidai ziliingia makubaliano na kuzikopesha kampuni hizo lakini hazijalipa mkopo huo na kwamba mpaka wakati wa kesi hiyo deni lilikuwa limefikia Dola 47,228, 592.53za Marekani.
Mahakama katika hukumu yake ilisomwa Ijumaa, Novemba 29, 2024 na Msajili, Joyce Minde kwa niaba ya Jaji Profesa Ubena Agatho aliyesikiliza kesi hiyo.
Jaji Agatho amesema baada ya kuchambua ushahidi wa pande zote ameridhika wadai waliashindwa kuthibitisha madai yao kwa kiwango kinachotakiwa na kwamba ushahidi wake si wa kuaminika.
“Itoshe tu kueleza hapa kwa kuzingatia uchambuzi na majibu ya hoja zilizotangulia, kesi ya wadai haijathibitishwa kwa kiwango kinachotakiwa, ambacho ni ulali wa uwezekano. Ni madai matupu bila ushahidi thabiti,” amesema Jaji Ubena na kusisitiza:
“Hivyo nafuuu pekee wanayostahili ni kufutwa kwa kesi yao. Kwa kusema hayo kesi ya wadai inafutiliwa mbali kwa gharama (kampuni hizo kuzilipa benki hizo gharama zilizozitumia kuendeaha kesi hiyo)”,
Badala yake Jaji Agatho amesema ushahidi wa wadaiwa (benki hizo) ni mzito na wa kuaminika na kwamba hivyo madai yao kinzani yana mashiko.
Jaji Agatho amerejea msimamo wa Mahakama ya Rufani katika moja ya rufaa ilizokwishakuziamua kuwa mikopo sharti irejeshwe vinginevyo benki na taasisi nyingine zinazotoa mikopo zitafilisika.
Hivyo, ametamka wakopaji (kampuni za Kahama na wenzake) wamekiuka vigezo na masharti ya mikopo na kwamba hibyo wadhamini (wao) na wanapaswa kuwajibika kikamilifu.
Hivyo, ameziamuru kampuni hizo na wadhamini wao katika mikopo huo kuzilipa benki hizo fidia ya hasara maalumu ya kiasi cha Dola 47,228,592.53 za Marekani ambazo ni jumla ya deni la msingi, riba na faini kwa mujibu wa makubaliano ya mikopo hiyo.
Pia, ameziamuru kampuni hizo kuzilipa benki hizo riba kwa kiwango cha Mahakama cha asilimia saba ya jumla kiasi hicho cha pesa yaani deni hilo kutoka tarehe hukumu mpaka tarehe ya kukamilisha malipo yote.
Wadhamini wa kampuni hizo katika mkopo huo, ambao pia walikuwa ni wadai katika kesi hiyo walikuwa ni kampuni za Kom Group of Companies Limited, Shinyanga Royal Pharmacy (2015) Limited, Royal Supermarket (2008) Limited na Mhoja Nkwabi Kabalo, mkurugenzi wa kampuni hizo.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo kampuni hizo ziliingia makubaliano ya mikopo na benki hizo yaliyosainiwa na pande zote kwa nyakati tofauti yaani Mei 28, 2018, Juni 19, 2020 na Desemba 22, 2022 na kampuni hizo zikapokea mkopo wa jumla ya Dola 38 milioni za Marekani.
Baada ya muda wa makubaliano ya kurejesha mkopo huo kupitia benki hizo ziliziandikia kampuni hizo barua ya kuzitaka kulipa mkopo huo, Dola 46,658,395.81za Marekani, zikijumuisha deni la msingi na riba kulingana na makubaliano ya mikopo hiyo.
Benki hizo badala ya kulipa mkopo huo, zilikwenda mahakamani zikafungua kesi zikipinga kudaiwa wala kukopeshwa na benki hizo kiasi chochote cha pesa.
Katika madai yake na kwenye ushahidi wake kampuni hizo zilikiri kuingia mikataba na benki hizo wa mkopo wa jumla ya Dola za Marekani 32 milioni.
Hata hivyo, zilidai benki hizo hazikutekeleza wajibu wake, kuzipatia mkopo huo, huku zikidai kuwa benki hizo zilitoa kiasi cha Dola 32 milioni kwa Kampuni ya Kom Group of Companies ya Nairobi Kenya.
Badala yake zilidai zilipokea mkopo wa Dola 30 milioni kutoka kwa Kom Group of Companies Limited ya Nairobi Kenya na si kwa wadaiwa (benki hizo) na kwamba tayari zilishaanza kulipa sehemu ya mkopo huo.
Hivyo ziliiomba Mahakama pamoja na mambo mengine itamke kuwa benki hizo zilikuwa na makubaliano, hivyo hazina madai yoyote dhidi yao na iamuru benki hizo zirejeshe dhamana na hatimiliki za dhamana za mkopo walizozikabidhi kwa benki hizo.
Benki hizo katika madai yake kinzani na katika ushahidi wake zilidai kuwa zilitimiza wajibu wake wa kimkataba lakini wadai hao (wakopaji) waliokiuka masharti ya mkataba wa mkopo, hivyo zinastahili kushikilia amana zote zilizowekwa kama dhamana ya mkopo huo.
Zilidai mpaka kufikia Julai 26, 2023 deni la msingi lilikuwa limeshafikia Dola za Marekani 47, 228,592.53, ikiwa ni deni la msingi, riba inayozidi kuongezeka na faini.
Zilifafanua Kom Group of Companies Limited of Nairobi Kenya, ambayo kampuni hizo zilidai kuwa ndiyo iliyozikopesha si kampuni bali ni jina la akaunti ambayo ziliifungua kwa ajili ya kuwezesha miamala ya mikopo hiyo kwa kampuni hizo.
Hivyo, zilizitaka kampuni hizo kutoa uthibitisho wa kuwepo kampuni hiyo yenye jina hilo.
Hivyo, ziliomba Mahakama iamuru kwamba wadai (kampuni hizo) wamekiuka vigezo na masharti ya mikataba hiyo ya mikopo uliosainiwa na pande zote na iamuru wakopaji hao na wadhamini wao kulipa jumla ya Dola 47, 228,592.53za Marekani.
Jaji Agatho katika hukumu hiyo ametupilia mbali madai na hoja za wadai badala yake amekubaliana na madai na hoja za wadaiwa.
Amesema madai kuwa wadaiwa hao hawakupokea pesa hizo kutoka kwa EBK bali kwa KOM Group of Companies Limited hayaaminiki kwa kuwa walishindwa kuthibitisha kuwepo kwa kampuni hiyo kama taasisi hai iliyosajiliwa.