Geita. Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) Mkoa wa Geita, limewatahadharisha wadau wote wa vyombo vya usafiri na wavuvi wanaotumia Ziwa Victoria, kufuatilia taarifa za hali ya hewa kabla ya kuanza safari za majini hususan kipindi hiki chenye mvua nyingi na upepo.
Ofisa Mfawidhi wa Tasac Mkoa wa Geita, Godfrey Chegere aliyasema hayo jana Novemba 26,2024 wakati akitoa elimu ya usalama kwa kuzingatia sheria na kanuni za usafiri majini, kwa abiria na wamiliki wa vyombo vya usafiri katika mwalo wa Makatani na Abiria iliyopo kata ya Nkome Wilaya ya Geita.
Chegere amesema Desemba huambatana na mvua na upope mkali, hivyo wamiliki wa vyombo na wanaoviendesha wanapaswa kuangalia taarifa za hali ya hewa kabla ya kuanza safari.
“Wamiliki wote wa vyombo na viongozi wa mialo tumeunda group la WhatsApp kwa ajili ya kupeana taarifa za hali ya hewa kutoka kwenye kitengo chetu cha hali ya hewa kilichopo Mwanza, kabla ya kuanza safari fika kwenye ofisi za hawa viongozi wa mwalo watakupa taarifa, kama kuna upepo nawasihi msiingie ziwani maana mawimbi yatakua makali,” amesema Chegere.
Katika hatua nyingine, Chegere amewataka wamiliki wa vyombo vya majini kuzingatia sheria kwa kubeba abiria kwa idadi inayolingana na uwezo wa chombo hicho.
“Chombo cha abiria kibaki kwa abiria na mizigo ibaki mizigo msibebe abiria na mizigo kwenye chombo kimoja hii ni hatari,” amesema Chegere.
Aidha, amewataka wavuvi na abiria kuhakikisha wakati wote wa safari wanavaa ‘lifejacket’ na kuzingatia sheria za usalama kwani ni kawaida katika kipindi cha msimu wa sikukuu, idadi ya abiria kuongezeka.
Akizungumzia ajali za majini, Chegere amesema utolewaji wa elimu ya usalama umesaidia kuzipunguza kwa kiwango kikubwa, kwa mwaka wa fedha uliopita, ziliripotiwa ajali tano na tangu mwaka huu uanze hakuna ajali iliyotokea.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati amewataka wamiliki wa vyombo vya usafiri majini kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni na utaratibu unaotumika kuongoza vyombo hivyo, huku akiwataka kuchukua tahadhari msimu huu wa sikukuu kwa kutobeba abiria zaidi ya uwezo wa chombo.
“Tasac fanyeni ukaguzi angalieni uzingatiaji wa sheria hasa kipindi hiki cha sikukuu ambacho wasafiri wanakuwa wengi, hakikisheni kuna vifaa vya uokozi karibu na wapakie abiria kulingana na uwezo wa chombo,”amesema Gombati.
Baraka Pantaleo mvuvi katika mwalo wa Makatani amesema elimu inayotolewa na Tasac pamoja na kaguzi wanazofanya mara kwa mara imesaidia kuondoa vyombo vibovu majini na vilivyopo kuwa na vifaa vya uokozi.
“Zamani ilikua mtumbwi ukizama kumpata mtu ni kazi na wakati mwingine mnamkuta ameshapoteza maisha lakini sasa hivi inakuwa rahisi ‘lifejacket’ inasaidia kumuona mtu mapema na kumuokoa,” amesema Pantaleo