Sababu Tanzania kuteuliwa WHO Afrika

Dar es Salaam. Kufanikiwa katika afua za afya ikiwamo miundombinu katika ngazi ya msingi, kupunguza vifo vya wajawazito na afya kwa wote ni miongoni mwa sifa za Tanzania kupewa nafasi ya kugombea nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika.

Nafasi hiyo ambayo ni mara ya kwanza kupewa nchi za Afrika Mashariki, Rais Samia Suluhu Hassan amemteua mbunge wa Kigamboni, Dar es Salaam na Mtaalamu wa Diplomasia ya Afya, Dk Faustine Ndugulile kugombea.

Wakizungumza leo Jumatano, Mei 8, 2024, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, January Makamba wamesema Dk Ndugulile ana uzoefu mkubwa wa masuala ya afya ya kidiplomasia na ujuzi mkubwa wa afya duniani na nchini.

Waziri Ummy amesema Tanzania imepewa nafasi hiyo kutokana na mafanikio kadhaa ambayo imepiga katika kufanikisha miundombinu ya afya ngazi za juu na katika afya ya msingi ikiwamo ujenzi wa vituo vya afya na kushusha huduma za msingi chini.

Ametaja sababu ya pili ni moja ya nchi zinazofanya vizuri barani Afrika katika kupambana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.

“Tumefanikiwa kupunguza vifo vya wajawazito kwa asilimia 80 japokuwa bado hatujaweza kufikia malengo katika vifo vya watoto wachanga hilo ni eneo ambalo ninaendelea kulipigania, lakini pia tumefanikiwa katika chanjo zikiwamo za watoto chini ya umri wa miaka mitano tunashika nafasi tatu za juu Barani Afrika,” amesema.

Amesema kupitia mafanikio hayo, Tanzania itatumia nafasi hiyo kutoa ujuzi, uzoefu mkubwa katika kutunga sera za afya kwa bara la Afrika na dunia kwa jumla.

Waziri Ummy amesema Tanzania haina historia ya kuwa na mgombea katika nafasi hiyo na viongozi watano kutoka nchi tano zikiwamo za Senegal, Ivory Coast, Niger, Rwanda na Tanzania zinashiriki kinyang’anyiro hicho.

Hata hivyo, amesema Dk Ndugulile ameteuliwa na Rais Samia kutokana na uwezo wake wa kuchanganua masuala ya afya ndani na nje ya nchi kwani amefanya mengi kwa Afrika kabla ya kuingia katika siasa lakini pia anaongoza nafasi kadhaa katika Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

“Nimefanya naye kazi tangu mwaka 2017 na alikuwa kiongozi mzuri, japokuwa yeye ni daktari na mimi mwanasheria alijitahidi kunielekeza na hakuweza kunivunjia heshima wakati wote, alinipa ushirikiano mkubwa wakati wa Uviko-19 na tulifanikiwa kuwaweka Watanzania salama,” amesema Waziri Ummy.

Naye Waziri Makamba amesema Wizara ya Afya na Mambo ya Nje walipata maelekezo na mwongozo kutoka kwa Rais wampendekeze Dk Ndugulile.

Amesema wanaamini atafanya kazi nzuri kuwa naye kama mshiriki wa nafasi hiyo anajua kazi, ana mawazo chanya na atafanya nchi ijivunie.

“Rais alivyoridhia jina lake liende lazima tuhakikishe anashinda, sisi katika siasa hakuna kinafanikiwa bila kampeni. Wapiga kura ni Mawaziri wa Afya kutoka nchi 47 na kwetu ushirikiano wa masuala ya afya kimataifa ni jambo muhimu sana, kama nchi tunampendekeza kwa nafasi hiyo,” amesema.

Makamba amesema katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu Jamhuri ya Demokrasia ya Congo(DRC), tayari Tanzania imepata kura za nchi zote za Kusini mwa Jangwa la Sahara yaani SADC.

“Tuna mtaji mkubwa  kama mwanachama wa SADC, tumepata barua rasmi nchi 16 zote za SADC zinatuunga mkono, nilipokuwa safari tulishaanza kampeni nchi 7 wametuahidi kutuunga mkono tuna kura 23 jumla tuna mtaji wa nusu ya kura nafasi yetu ni nzuri, sifa na heshima ya Tanzania itadhihirika katika uchaguzi huu ,” amesema.

Makamba amesema kazi kubwa iliyofanyika katika mageuzi makubwa kwenye afya itaibeba nchi katika sera, mipango na mifumo ya afya iliyowekwa.

“Kigamboni watakukosa, lakini Afrika watapata jembe. Dk Ndugulile ametumika hapa nchini na sasa anakwenda kutumikia nafasi nyingine iwapo kura zitaamua,” amesema Makamba.

Kauli ya Waziri Makamba ingawa hakuifafanua yeye mwenyewe na hata swali lilipoulizwa iwapo atashinda nafasi hiyo kama kuna uwezekano wa kuendelea na ubunge inaashiria jimbo hilo likawa wazi na kuruhusu mgombea mpya wa CCM.

Ndugulile ataja vipaumbele saba

Akitoa neno la kushukuru, Dk Ndugulile alitoa vipaumbele saba ambavyo ataanza navyo, ikiwa ni sehemu yake ya kujinadi kabla ya uchaguzi baadaye Agosti.

Amesema atahakikisha suala la afya kwa wote linanyiwa mkazo kwa vitendo kwa kuwafikia wananchi wote akisema, Tanzania imefanikiwa katika mchakato wa bima ya afya kwa wote kwa kupiga hatua kubwa katika uboreshaji wa hilo ikiwemo afya ya msingi.

Ametaja kipaumbele kingine kuwa ni kupunguza vifo vya mama na mtoto ikiwa ni miongoni mwa mambo muhimu kwa WHO.

“Tutasimamia kujenga mifumo ya afya imara, tunaona mifumo mingi imeathirika na vita na majannga mengine zikiwemo mvua za El -Nino.

“Magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa changamoto kubwa, mimi ni daktari na mtu wateknolojia tunataka kuangalia namna gani tutafanya ugunduzi na kutibu kwa kutumia teknolojia,” amesema Dk Ndugulile.

Machi 11, 2023, Dk Faustine Ndugulile aliteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya ushauri masuala ya afya ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Kwa uteuzi huo unaofanywa na Rais wa umoja huo wa mabunge duniani, ulimfanya Dk Ndugulile kuwa sehemu ya wabunge 12 duniani wanaoishauri IPU kuhusu masuala mbali mbali yanayohusu afya.

Uteuzi huo ulianza Februari mwaka 2023 ambao utadumu miaka minne.

Oktoba 24, 2023 Dk Ndugulile alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati ya ushauri ya masuala ya afya ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika uchaguzi uliofanyika Jijini Luanda nchini Angola.

Kamati ya ushauri ya masuala ya afya, ina majukumu ya kushauri mabunge ya nchi na umoja wa mabunge duniani kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu afya.

Related Posts