Serikali yawatwisha jukumu la ajira wathibiti ubora wa shule

Arusha. Ili kukabiliana na changamoto ya wahitimu wa elimu nchini kushindwa kupata ajira kutokana na ukosefu wa ujuzi, Serikali imewaagiza wathibiti ubora wa shule kuhakikisha utekelezaji wa mtalaa wa amali unafanyika ipasavyo.

Mtalaa huo unalenga kuwajengea vijana ujuzi wa vitendo, ili waweze kushindana katika soko la ajira.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA), imebainisha kuwa zaidi ya asilimia 61 ya wahitimu wa vyuo nchini wanakosa ajira, hasa katika sekta muhimu za huduma kutokana na ukosefu wa ujuzi.

Hali hiyo imeifanya Serikali kufanya mageuzi katika mfumo wa elimu kwa kuanzisha mtalaa wa amali mwaka 2023 unaotoa kipaumbele kwa elimu ya vitendo kuliko nadharia.

Mkurugenzi wa idara ya udhibiti ubora wa shule, Ephraim Simbeye akizungumza leo Jumapili, Desemba mosi, 2024 jijini Arusha amesema katika dunia ya sasa inayokabiliwa na mabadiliko ya kiteknolojia na mahitaji ya soko la ajira yanayobadilika kwa kasi, elimu ya ujuzi ni muhimu zaidi kuliko nadharia.

Amesema hayo kwenye mafunzo ya siku tatu kwa wataalamu wa uthibiti ubora wa shule 340 kutoka mikoa yote ya Tanzania.

Simbeye amesisitiza kuwa mabadiliko hayo yanawapa vijana uwezo wa kujitegemea kiuchumi kupitia ajira au bunifu za kiteknolojia, hivyo kuchangia maendeleo ya Taifa.

Amewataka washiriki kuhakikisha utekelezaji wa mtalaa wa amali unafanyika kwa ufanisi, ili wahitimu wawe na uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko la ajira kitaifa na kimataifa.

“Nendeni mkatekeleze majukumu yenu kwa ufanisi, kuhakikisha tunapata vijana waliobobea katika ujuzi wa vitendo ambao wanaweza kubadilisha changamoto za jamii kuwa fursa za kiuchumi,” amesema.

Kwa upande wake, Kamishna wa Elimu, Dk Lyambwene Mtahabwa amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea wataalamu mbinu bora za kusimamia utekelezaji wa mtalaa wa amali, huku wakisaidia walimu wakuu na wasimamizi wa shule kuelewa mtalaa, ili kuleta matokeo chanya.

Mthibiti ubora wa shule kutoka wilaya ya Muheza, Theresia Kapinga amesema utekelezaji wa mtalaa wa amali utasaidia kuzalisha wataalamu wa kutosha kwenye soko la ajira, huku pia ukikuza bunifu zinazotatua changamoto za jamii.

“Mtalaa huu ukitekelezwa ipasavyo utaleta mabadiliko makubwa, kwani vijana watapata ujuzi wa kubadilisha changamoto kuwa fursa za kiuchumi,” amesema.

Related Posts