Ubunifu kiteknolojia unavyopunguza hasara katika kilimo

Ndoto ya kila mkulima ni kupata mazao mengi ili aingize fedha za kutosha, lakini wakati mwingine msimu wa mavuno, hasa kwa wakulima wa mbogamboga na matunda huacha majonzi.

Majonzi hayo yanatokana na kukosa soko na wakati mwingine bei ndogo wanayokutana nayo sokoni na hofu ya kupoteza mali baada ya mazao kuharibikia shambani, ambayo humlazimu mkulima kuuza mazao yake kwa bei chee.

Takwimu za mkakati wa usimamizi wa mazao baada ya kuvuna zilizotolewa na Wizara ya Kilimo zinaonyesha kuwa takribani asilimia 30 hadi 40 ya nafaka zinazozalishwa kila mwaka nchini huharibika kabla ya kufika sokoni, huku hali ikiwa mbaya zaidi kwa bidhaa za matunda na mbogamboga.

Lakini changamoto hizo zinasababishwa na kukosekana kwa teknolojia rafiki na nafuu ambazo zinaweza kuwasaidia kuhifadhi mazao yao kwa ajili ya soko la baadaye ambapo uhitaji wa bidhaa hiyo sokoni utakuwa mkubwa.

“Kuna wakati niliwekeza zaidi ya Sh14 milioni kwenye kilimo cha nyanya, zilistawi, kila nikija shambani nilijua ni wakati wangu wa kuaga umasikini. Lakini kila aliyelima kipindi hicho alivuna kwa kiasi kikubwa, jambo ambalo liliifanya bei kuporomoka sana. Boksi moja tukawa tunauza Sh10,000 hadi kwa Sh14,000,” anasema Mathayo Mmasi, mkulima wa nyanya na vitunguu kutoka kijiji cha Imbaseni, mkoani Arusha.

Bei ikiwa nzuri muuzaji wa jumla anaweza kuuziwa Sh35,000 kwa boksi moja, inategemeana na mahitaji yaliyopo sokoni na uzalishaji.

Anasema hali hiyo ilisababishwa na kukosekana kwa uhakika wa muda ambao bidhaa hizo zinaweza kudumu shambani kabla ya kuharibika, jambo ambalo liliwalazimu kuuza kwa hasara ili kuepuka kupoteza fedha zaidi.

“Sawa tunauza boksi nyingi, lakini kiuhalisia kama bei ingekuwa nzuri sokoni, tungepata pesa nyingi. Unaona faida ya ulichokifanya hata unapata moyo wa kulima tena na tena,” anasema.

Maneno yake yanaungwa mkono na Maria Sekei, ambaye pia ni mkulima kijijini hapo, anayetamani teknolojia za uongezaji thamani za bei nafuu zipatikane ili kuondoa kero wanayokutana nayo ya kuuza mazao kwa bei ya hasara ili yatoke.

Kutokana na changamoto zinazowakumba wakulima wa mazao ya nyanya na mengine ambayo ni rahisi kuharibika, George Nyahende alibuni mashine inayotumia umeme jua inayoweza kuongeza thamani katika bidhaa za mbogamboga na matunda.

Alibuni mashine hiyo baada ya kuoa adha wanayopitia wakulima wa bidhaa hizo mkoani kwake, huku akilenga kuwakwamua kiuchumi.

Nyahende ni mhitimu wa Veta Arusha na amebuni mashine ambayo mkulima wa vitunguu, nyanya au mbogamboga na matunda anaweza kukausha mazao yake na kuyahifadhi sehemu akisubiri soko la baadaye ambalo linaweza kuwa na faida kwake, tofauti na msimu wa mavuno mengi.

Mbali na kukausha, mbunifu huyu alienda mbali zaidi na kuwawezesha kusaga bidhaa zao kwa wale wanaohitaji ili waweze kuziuza kadiri soko linavyostawi.

“Hii nililenga kuwafungulia wigo zaidi wa soko, wasiangalie soko la ndani pekee, bali na lile la kimataifa kupitia bidhaa zao hizo, kwani watakuwa wameziongezea thamani. Hawatakuwa na hofu ya mazao kuharibika kabla hayajafika sokoni kama ilivyo sasa,” anasema.

Nyahende anaamini njia hii kuwa bora, kwani itawasaidia kufanya shughuli zao bila kutegemea nishati ya umeme au mafuta ambayo ni gharama na badala yake watatumia nishati ya jua.

“Kuongeza thamani ndiyo dunia inakokwenda, hii haitaongeza tu fedha kwa wakulima, bali pia itasaidia kupambana na upotevu wa mazao katika kilimo, hivyo tija itaongezeka na Serikali itapata mapato zaidi,” anasema.

Hata hivyo, licha ya ubunifu huo kuonyesha kuwa mkombozi wa wengi kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, umekuwa ukiishia katika maonyesho mbalimbali bila kupata fedha ya kuliendeleza kwa ajili ya matumizi ya baadaye.

Nyahende anawakilisha kundi kubwa la wabunifu wa teknolojia mbalimbali za kuongeza thamani ya mazao kwa kutumia umeme jua ambazo licha ya kuwa na uwezo wa kuongeza tija katika kilimo, bado halijafanikiwa kupata fedha kwa ajili ya uzalishaji ili kuwafikia wakulima.

Hali hii nawafanya wakulima kuendelea kuuza bidhaa zao kwa hasara kutokana na wigo mdogo walionao katika kuyafikia masoko na wanunuzi kwa jumla.

Takwimu zinaonyesha kuwa mawazo bunifu kutoka Tanzania yanavutia uwekezaji kutoka nje kwa kiwango kidogo ikilinganishwa na wenzetu, ikiwemo Kenya.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Tanzania startups Association (TSA), mwaka 2023, mawazo bunifu kutoka Afrika yalivutia mtaji wa zaidi ya Sh7.37 trilioni, lakini katika fedha hizo, Tanzania iliambulia Sh63.750 bilioni pekee.

Hata hivyo, mbali na kusubiri uwekezaji kutoka nje, Tanzania pia imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha.

Moja ya wanaowezesha wakulima ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ambayo imepewa dhamana kusimamia sekta hii.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wake, Frank Nyabundege, pamoja na kutoa mikopo kwa wakulima, pia wamekuwa wakitoa mikopo kwa wabunifu ili waweze kuendeleza mawazo yao.

“Ndiyo kazi yetu, mtu anakuwa na wazo linatengenezwa, linafadhiliwa na mradi unaendelezwa, wanachotakiwa kufanya kama mtu ana wazo linalohusu kilimo awasilishe maombi kwetu halafu sisi tutayapitia ili aweze kupewa mkopo,” anasema Nyabundege, huku akiweka wazi kuwa yapo mawazo yaliyopewa ufadhili huo.

Si benki hiyo tu, bali pia CRDB kupitia programu yake ya Imbeju imekuwa ikiwezesha wabunifu mbalimbali kufikia malengo yao.

Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), nao mwaka jana walitoa takribani Sh4 bilioni kwa mawazo bunifu.

Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Amos Nungu anasema bunifu za umeme jua zimekuwa na manufaa katika kuongeza tija katika kilimo, kwani unapatikana muda wote, ni suala la mtu kuweza kuvuna.

Hilo linafanyika bila gharama nyingine yoyote ambayo mtu anapaswa kuitumia katika kufanya uzalishaji.

“Kitu kinachohangaikiwa ni ubunifu unakuja na kitu kipya au umekiboresha, kama akija na wazo au kuboresha kuvuna umeme jua tunahamasisha matumizi yake kwa sababu wanatatua changamoto katika jamii na sisi Costech tunawafundisha wafanye bunifu zenye tija,” anasema.

Anasema kupitia hilo, kama Serikali imekuwa ikisaidia kupata ufadhili kwa wabunifu hao ili mawazo hayo yawe makubwa kwa ajili ya kusaidia wananchi.

Anasema hilo linafanyika kuendana na mahitaji ya wananchi kwanza na kusaidia kutekeleza mahitaji ya Serikali.

Alitolea mfano wa vijana wanne waliotoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao wamebuni mbolea asili kwa kutumia mabaki ya chakula ambayo inatumika katika kilimo cha parachichi na wameisajili Umoja wa Ulaya, jambo ambalo huweka urahisi kwa wakulima kuuza mazao yao nje ya nchi.

Related Posts