Arusha. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametangaza uamuzi wa kuunda tume mbili ikiwamo itakayochunguza na kutoa mapendakezo kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa Ngorongoro.
Nyingine itaangalia utekelezaji wa uhamaji kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Msomera, wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.
Rais Samia ametangaza uamuzi huo leo Jumapili, Desemba mosi, 2024 Ikulu ndogo ya Arusha alipozungumza na viongozi wa kimila wa jamii ya kimasai (Malaigwanani) wanaoishi eneo la Ngorongoro.
Lengo lilikuwa kuwasikiliza viongozi hao kutokana na kuwepo malalamiko kuhusu baadhi ya uamuzi wa Serikali kuhusu eneo la Ngorongoro.
Katika kikao hicho kilichokuwa cha ndani, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais-Ikulu imesema, Rais Samia amewahakikishia Serikali itaendelea kuimarisha utendaji kazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na jamii hiyo.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameitaka Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kushughulikia changamoto zinazojitokeza, ikiwamo kukosekana kwa baadhi ya huduma za msingi za kijamii katika eneo la Ngorongoro.
Rais Samia amekutana na jamii hiyo ya Kimaasai ambayo imekuwa na malalamiko mbalimbali ikiwamo shughuli hiyo ya kuhamishwa na kusitishwa kwa huduma za kijamii elimu, afya, maji na kuondolewa vikwazo vya kuingia na kutoka eneo hilo.
Kikao hicho kimehudhuriwa na mawaziri zaidi ya kumi ambao ni, William Lukuvi (Sera, Bunge na Uratibu), Abdallah Ulega (Mifugo na Uvuvi), Stergomena Tax (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Dk Pindi Chana (Maliasili na Utalii), Profesa Palamagamba Kabudi (Katiba na Sheria) na Dk Mwigulu Nchemba wa Fedha.
Wengine ni, Hamad Masauni (Mambo ya Ndani), Mohamed Mchengerwa (Tamisemi), Hussein Bashe (Kilimo), Jumaa Aweso (Maji) na Innocent Bashungwa (Ujenzi). Pia, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda na Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Thomas Ole Sabaya walikuwa miongoni mwa walioshiriki.
Malalamiko mengine yaliyosababisha maandamano kwa siku tano eneo hilo la Tarafa ya Ngorongoro ni kupinga kufutwa vitongoji 96, vijiji 25 na kata 11, amri ambayo kimsingi ilikuwa ikiwakosesha haki ya kupiga kura.
Hatua hiyo iliifanya Serikali Agosti 23, 2024 kuwatuma mawaziri kwenda kuzungumza na wananchi wa kata 11, katika eneo la Oloirobi lililopo Kata ya Ngorongoro ambao walikuwa eneo hilo tangu Agosti 18, 2024.
Mawaziri waliokwenda ni William Lukuvi (Sera, Bunge na Uratibu), Profesa Palamagamba Kabudi (Katiba na Sheria) na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Danstan Kitandula.
Pia, walikuwapo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadh Juma Haji.
Akizungumza na mamia ya wananchi hao siku hiyo, Lukuvi alisema Rais Samia aliagiza kurejeshwa huduma za kijamii, kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa na kuondolewa vikwazo vyote vilivyowekwa kwa wakazi wa Tarafa ya Ngorongoro.
Alisema Rais Samia alikuwa na taarifa wananchi hao hawapati baadhi ya huduma zikiwamo za kuharibika kwa miundombinu kama vyoo vya shule, hali inayosababisha wanafunzi kujisaidia vichakani.
Katika kutekeleza hilo, uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024 vijiji na vitongoji vyote vya Ngorongoro ambayo awali vilikuwa vimefutwa navyo vilishiriki uchaguzi huo.
Kuhusu huduma za kijamii, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Novemba 18, 2024, ulimpongeza Rais Samia kwa hatua nzuri aliyoichukua ya kutuma wajumbe wake na kurejeshwa kwa huduma za kijamii kwa wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro.
Mratibu Taifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa katika taarifa yake kwa umma juu ya kinachoendelea Ngorongoro alisema huduma mbalimbali za jamii kama vile za mabweni kwa shule za msingi na sekondari, huduma za vyoo mashuleni, afya, barabara, huduma za maji, vibali vya ujenzi na huduma nyinginezo zilififishwa.
“Pamoja na kwamba Serikali ndio imelalamikiwa kusababisha changamoto hizi, kitendo cha Rais kuamua vikwazo hivi viondolewe imeleta matumaini mapya kwa watu wa Ngorongoro, kimetufurahisha sisi watetezi wa haki za binadamu na pia hatua hii inalinda taswira ya nchi katika eneo la haki za binadamu na utawala bora,” amesema.
Olengurumwa alisema kwa muda mrefu watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakishauri uongozi wa juu wa nchi ukutane na wananchi na mara baada ya Rais kutuma wajumbe wake, wameanza kuona faida ya hatua hiyo.
Hadi Mei 26, 2024, aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi alieleza waandishi wa habari awamu ya kwanza ya waliohama kwa hiari eneo hilo ilianza Juni 16, 2022 na hadi Januari 18,2023 , jumla ya kaya 551 zenye watu 3,010 zilihama.
Kati ya hizo, kaya 503 zenye watu 2,692 zilihamia Msomea na 48 zenye watu 318 kwenye maeneo mengine nchini, katika mikoa zaidi ya nane na kaya zote hizo zilikuwa na mifugo 15,321.
Alisema awamu ya pili ilianza Agosti 24, 2023 hadi Aprili 28, 2023 ilihusisha kata 822 zenye watu 5,354.
“Katika awamu zote mbili tangu mpango huo uanze kaya 1, 373 zenye watu 8,364 zimeshahama ambapo kijiji cha Msomera kimepokea kata 1, 248 zenye watu 7,547 na maeneo mengine kata 125 zenye watu 81 na mifungo jumla iliyohamishwa ni 36, 457,” alisema.