Profesa Janabi asimulia alivyosimamia mitihani ya Dk Ndugulile

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi amesema anachokikumbuka kwa aliyekuwa mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile ni jinsi alivyomsimamia mitihani miwili kwa nyakati tofauti.

Hayo amebainisha alipojitokeza kuomboleza na kuhani msiba wa Dk Faustine Ndugulile nyumbani kwake Kigamboni jijini Dar es Salaam leo Jumapili, Desemba 1, 2024.

Dk Ndugulile alifikwa na mauti usiku wa kumkia Jumatano ya Novemba 27, 2024 nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.

Mwili wake utaagwa kesho Jumatatu, katika viwanja vya Karimejee na kuzikwa Jumanne, Desemba 3, 2024 makaburi ya Mwongozo Kigamboni.

Akizungumza mbele ya waombolezaji nyumbani hapo, Profesa Janabi amesema:”Kwanza kabisa nimesimama hapa kama Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili sehemu ambayo marehemu alifanya kazi, sasa namfahamu na nakumbuka sijuhi bahati nzuri au mbaya nilimsimamia mtihani ilikuwa mwaka 1994 na 1995 mimi niliwahi kidogo kusoma.

“Kila mwanafunzi akifanya mtihani huwa anataka kujua majibu yake na aliponifuata nilimkatalia sitoi majibu labda wafuate viongozi na baada ya hapo alifanya internship (mafunzo kwa vitendo) yake akamaliza na mimi nilikuwa naenda zangu nje kusomea PhD (udaktari),” amesema.

Profesa Janabi amesimulia bahati mbaya nyingine na Dk Ndugulile ni mwaka 2001 wakati anafanya mtihani mwingine alikuwa anamsimamia:”Hapa siwezi kusema yaliyotokea kwenye mitihani lakini mjue dunia inakwenda haraka.” Kauli hiyo iliibua vicheko kutoka kwa waombolezaji nyumbani hapo.

Katika maelezo yake, Profesa Janabi amesema baada ya hapo akawa daktari na alikuwa akizungumza naye mara kwa mara na msisitizo kwake alikuwa akimtaka afanye PhD jambo alilomkubalia.

“Ghafla 2010 alikuja kuniambia anaingia kwenye ulingo wa kisiasa na hiyo ilikuja baada ya kumaliza masomo yake Afrika ya Kusini, baada ya kuingia huko kila mmoja anajua mafanikio aliyoyapata,” amesema.

Profesa Janabi amesema hata mke wa Dk Ndugulile alipata nafasi ya kumfundisha na hata alipopata taarifa ya msiba huo ilimshtua zaidi.

“Kinachoniumiza zaidi Dk Mwere Malecela alikuwa WHO naye tulimpoteza, tuliposikia kuhusu Ndugulile muda mchache kabla ya kuanza kazi kwakweli imenisikitisha,” amesema.

Dk Mwele alikuwa Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele katika WHO ambaye alifariki dunia Alhamisi ya Februari 10, 2022 mjini Geneva, Uswisi wakati akipatiwa matibabu.

Profesa Janabi amesema Dk Ndugulile ni mtu aliyeondoka nchini mwenyewe kwenda nchini India si kwamba alikuwa kwenye gari ya wagonjwa:”Sasa kusikia mmepoteza inakuwa ni mshtuko mkubwa.”

“Nchi imepoteza hasa kwa hizi nafasi ambazo zingetuweka kwenye ramani ya dunia hasa sekta ya afya ni ngumu binafsi naweza kudhibitisha hili kwakuwa nipo katika sekta hii kwa muda mrefu,” amesema.

Agosti 27, 2024, Dk Ndugulile alichaguliwa kuwa Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika na alitarajiwa kuanza kutumia nafasi hiyo mpya kwake Februari/Machi 2025.

Profesa Janabi amesema hata nafasi ya kwanza ya Dk Mwele anayeweza kuwa shuhuda mzuri ni mbunge wa Tanga Mjini na aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alivyoshiriki.

“Kikubwa yote ni mapenzi ya Mungu, na ujumbe wangu kwa sote tuliobaki tuangalie afya zetu kwa kwenda kupima mara kwa mara kujua afya zetu na kila mtu anajijua kuna wanaotakiwa kila mwaka na wengine kila mwezi ugonjwa ukigundulika mapema inakuwa rahisi kuanza matibabu,” amesema.

Related Posts