Hivi ndivyo Nondo wa ACT Wazalendo alivyotekwa Dar

Dar es Salaam. Wakati tukio la Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Abdul Nondo kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana likiibua mjadala, Jeshi la Polisi limeelezea jinsi tukio hilo lilivyotokea.

Nondo anadaiwa kukutwa na kadhia hiyo leo Jumapili, Desemba mosi, 2024 muda mfupi baada ya kushuka katika basi kituo cha mabasi cha Magufuli, jijini Dar es Salaam akitokea mkoani Kigoma alikokuwa akishiriki shughuli za chama hasa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Novemba 27, 2024

Baada ya kusambaa kwa taarifa hiyo, leo saa 6 mchana, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Msime ametoa taarifa kwa umma akielezea tukio hilo lilivyokuwa kwa mujibu wa mashuhuda.

 “Jeshi la Polisi lingependa kujulisha, Desemba mosi, 2024 saa 11.00 alfajiri katika eneo la stendi ya Magufuli Mbezi Louis, Dar es Salaam kuna mtu mmoja mwanamume amekamatwa kwa nguvu na kuchukuliwa na watu waliokuwa wakitumia gari lenye usajili wa namba T 249 CMV aina ya Land Cruiser rangi nyeupe.

“Ilielezwa na mashuhuda katika purukushani za ukamataji begi dogo lilidondoshwa na baadhi ya vitu vilivyokuwemo vimetambuliwa ni vya Abdul Omary Nondo,” imeeleza taarifa hiyo.

Misime amesema ufuatiliaji wa tukio hilo ulianza baada ya kupokewa taarifa hiyo pamoja na kufungua jalada la uchunguzi.

Tukio hilo limetokea ikiwa zimepita siku 86 tangu tukio kama hilo lilipotokea eneo la Tegeta, mbele ya Jengo la Kibo Complex, jijini Dar es Salaam kwa watu wenye silaha kuingia ndani ya basi la Kampuni ya Tashrif na kumchukua mwanachama wa Chadema, Ali Kibao.

Wakati wadau mbalimbali, ikiwamo Chadema wakipaza sauti za kumtafuta Kibao, asubuhi ya Septemba 8, 2024 taarifa katika mitandao ya kijamii, zilieleza mwili wa kada huyo ulitupwa Ununio jijini Dar es Salaam, huku usoni akiwa amejeruhiwa kiasi cha kutoonekana vema.

Machi 2018, Nondo akiwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) alidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana, kisha kutelekezwa wilayani Mufindi, Mkoa wa Iringa.

Baada ya tukio hilo, Naibu Katibu wa Haki za Binadamu na Vyombo vya Uwakilishi wa Wananchi wa ACT-Wazalendo, Mbarala Maharagande ametoa taarifa kwa umma akieleza Nondo ametekwa asubuhi akitokea Kigoma alikokuwa sehemu ya viongozi wa kitaifa walioongoza kampeni kwenye mikoa ya Magharibi mwa Tanzania.

“Mashuhuda wa tukio wanasema kulikuwa na purukushani katika utekaji wa Nondo iliyosababisha begi lake ndogo kudondoka. Katibu Mwenezi wa ACT- Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala na ofisa wa harakati na matukio, Wiston Mogha walifika mapema kituoni hapo, walitambua aliyetekwa ni Nondo kwa sababu walizitambua nguo zake kwenye begi lililodondoka na ‘note book’ yake,” amedai Maharagande kupitia taarifa hiyo.

Akizungumzia tukio hilo leo alasiri akiwa makao makuu ya ACT-Wazalendo, Magomeni, Dar es Salaam, Maharagande akiwa na wanachama wa chama hicho ametoa wito kwa kuachiwa kwa Nondo.

 “Tunatoa wito Nondo aachiwe au afikishwe kwenye vyombo vya sheria ajitetea kama ana kesi ya kujibu kutokana na kosa walilomkamatia,” amesema Maharagande alipozungumza na waandishi wa habari na kuongeza:

“Tunatoa wito kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), pamoja na kwamba jeshi limetoa taarifa ya kufuatilia, Nondo aachiwe au afikishwe kwenye vyombo vya sheria aweze kujitetea kama ana kesi ya kujibu kutokana na kosa walilomkamatia,” amesema.

Ameeleza watu waliomkamata waliokuwa wamevaa kiraia, huku wakiwa na gari pamoja na pingu.

Hivi karibuni Katibu wa Umoja wa Vijana Chadema (Bavicha), Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka na wenzake wawili, Jacob Mlay na Frank Mbise, walitoweka tangu Agosti 2024.

Kiongozi wa Chadema, wilaya ya Sumbawanga, Rukwa, Dioniz Kipanya, naye inadaiwa alitekwa. Wote hao mpaka sasa hawajulikani walipo.

Mbali na hao, raia wengine zaidi ya 80 wanadaiwa kutoweka na baadhi yao kuuawa na wasiojulikana, kama ilivyoripotiwa Agosti 2024 na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Wito wa uchunguzi kuwabaini wahusika na kuundwa tume ya kijaji itakayochunguza matukio yote kwa jumla, umekuwa ukitolewa na wadau wa haki za binadamu, wanasiasa na wanaharakati nchini.

Hata hivyo, wadau wanatoa wito huo wakati tayari Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), ilishaanza uchunguzi wa matukio ya namna hiyo.

Related Posts