YANGA imeshinda mechi yake ya kwanza chini ya kocha Sead Ramovic, ushindi ulioshusha presha kwa mashabiki wa timu hiyo lakini kocha wa watani wao Fadlu Davids amefunguka juu ya anayoyajua kuhusu Mjerumani huyo.
Yanga iliichapa Namungo juzi kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Majaliwa, mabingwa watetezi wakiendeleza rekodi ya kibabe mbele ya timu hiyo ukiwa ni ushindi wa sita kwenye mechi 11 walizokutana.
Kabla ya ushindi huu Yanga ilikuwa imepoteza michezo mitatu mfululizo katika mashindano tofauti dhidi ya Azam na Tabora United kwenye Ligi Kuu na Al Hilal kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ushindi wa juzi umewapa mashabiki wa timu hiyo imani kuwa kikosi chao chini ya Ramovic ambaye huu ulikuwa mchezo wake wa pili madarakani anaweza kufanya mambo makubwa kwenye michezo ijayo.
Akizungumza na Mwanaspoti kwenye mahojiano maalum, kocha wa Simba, Fadlu ambaye ni kocha kijana kama alivyo Ramovic, alisema anamfahamu vyema Mjerumani huyo wa Yanga na kwamba wawili hao ni marafiki wanaofahamiana hata kabla ya kuja kukutana hapa Tanzania wakizifundisha timu mbili kubwa tofauti, lakini akisema Yanga imepata kocha sahihi.
Fadlu alisema Ramovic ni kocha sahihi kwa Yanga na kwamba anajua falsafa zake anazotaka timu yake icheze soka la kushambulia.
“Sead Ramovic ni rafiki yangu, ni kocha mzuri nadhani (Yanga) wamempata kocha mzuri lakini hata Gamondi (Miguel) alikuwa kocha sahihi mzuri pia, anataka (Fadlu) timu yake icheze soka la kushambulia,” alisema Fadlu.
“Nadhani ana timu yenye wachezaji wazuri pia italeta ushindani mzuri baina yetu kwenye klabu ambazo tunazifanyia kazi, yeye na mimi ni makocha ambao tunafahamiana.”
Hata hivyo, Fadlu amewataka Yanga kumpa muda kocha wao huyo ili aweze kubadilisha mambo kwenye kikosi hicho kulingana na falsafa anazozitaka.
“Nadhani wanatakiwa kumpa muda ili aweze kufanya yale ambayo anataka timu yake iyafanye, anahitaji kufanyia kazi mambo ambayo anayahitaji kuyabadilisha kulingana na aina ya mpira anaoutaka timu yake icheze, haiwezi kuwa haraka, kwangu naamini ni kocha bora sana na mbinu zake ni hatari kwa wapinzani,” alisema Fadlu.
Kocha huyo anatarajiwa kufuatana na Yanga wiki hii kwenda Algeria kwenye mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wanapokwenda kuvaana na MC Alger Jumamosi ijayo mechi itakayopigwa saa 4:00 usiku.
Kabla ya kujiunga na Yanga, Ramovic alikuwa akiifundisha TS Galaxy ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), akiiwezesha timu hiyo kucheza soka la kiwango cha juu na kuzipa wakati mgumu timu kubwa za nchini humo zinazoogopwa.
Baadhi ya matokeo ya mechi za TS Galaxy ya Ramovic za Ligi Kuu ya Afrika Kusini msimu uliopita dhidi ya klabu kubwa:
JUMAMOSI, Aprili 6, 2024
SuperSport United 0 – 1 TS Galaxy
JUMANNE, Mei 7
Kaizer Chiefs 2 – 2 TS Galaxy
JUMAMOSI, Mei 18
TS Galaxy 1 – 0 Orlando Pirates
JUMANNE, Mei 21
TS Galaxy 1 – 1 Mamelodi Sundowns FC