Biden amsamehe mwanawe Hunter mashtaka ya jinai – DW – 02.12.2024

Kwa hatua hiyo, Rais Biden amekwenda kinyume na ahadi yake ya awali ya kutotumia nguvu zake za urais kwa manufaa ya familia yake.

Katika taarifa iliyotolewa jioni ya Jumapili, Biden alisema, “nauamini mfumo wa sheria, ila kwa kuwa nimepambana na hili, naamini pia kwamba siasa zimeingia kati katika kesi hii na zimepelekea kutopatikana kwa haki.”

“Madai katika kesi yake yametokea tu baada ya wapinzani wangu kadhaa wa kisiasa katika Congress kuyatumia kunishambulia na kupinga kuchaguliwa kwangu,” aliongeza Biden. “Hakuna mtu yeyote mwenye busara atakayeutazama ukweli katika kesi ya Hunter, atakayefikia maamuzi mengine mbali na kuwa Hunter alilengwa kwa kuwa ni mwanangu.”

“Natumai raia wa Marekani wataelewa kwanini baba na rais atafikia uamuzi huu,” aliongeza Biden.

Kuheshimu utawala wa sheria

Haya yanajiri wakati ambapo Hunter Biden alikuwa anatarajiwa kuhukumiwa katika wiki chache zijazo na chini ya miezi miwili kabla rais mteule wa Marekani Donald Trump kuchukua hatamu za uongozi.

Rais mteule wa Marekani Donald Trump
Rais mteule wa Marekani Donald TrumpPicha: Brandon Bell/Pool via REUTERS

Hatua hii inafikisha mwisho gumzo la muda mrefu kuhusiana na mwanawe Biden, ambaye mwezi mmoja baada ya babake kushinda uchaguzi wa mwaka 2020, alifichua hadharani kwamba alikuwa anachunguzwa.

Rais Biden aliapa mbele ya Wamarekani mara kadhaa kwamba ataheshimu utawala wa sheria baada ya muhula wa kwanza wa Trump, ila kwa sasa amekwenda kinyume na ahadi hiyo.

Mnamo mwezi Juni, Biden aliondoa uwezekano wa kumsamehe mwanawe au kupindua uamuzi wa mahakama, akiwaambia waandishi wa habari wakati Hunter alipokuwa akikabiliwa na kesi hiyo ya umiliki wa bunduki huko Delaware kwamba, “naheshimu uamuzi wa majaji. Nitafanya hivyo na sitamsamehe.”

Mnamo Novemba 8 baada ya ushindi wa Trump, msemaji wa ikulu ya White House Karine Jean-Pierre aliondoa uwezekano wa msamaha kwa Hunter akisema, “tumeulizwa swali hili mara kadhaa. Jawabu letu bado ni lile lile, hapana.”

Biden amekuwa akimuunga mkono huyo mwanawe wa pekee wa kiume aliye hai, kwani Hunter aliingilia matumizi ya madawa ya kulevya na kuyaharibu maisha yake na ya familia yake, kabla kujiondoa kutoka kwenye matumizi ya madawa hayo katika miaka ya hivi karibuni.

Taarifa za uongo

Kwa miaka sasa, wapinzani wa kisiasa wa Biden wamekuwa wakiyatumia makosa ya mwanawe kumshambulia na kumkosoa.  

Biden akiwa na mwanawe Hunter huko Massachusetts
Biden akiwa na mwanawe Hunter huko MassachusettsPicha: Craig Hudson/REUTERS

Hunter Biden alifunguliwa mashtaka mnamo mwezi Juni katika mahakama ya shirikisho ya Delaware kwa makosa matatu ya kununua bunduki mwaka 2018, waendesha mashtaka wakisema, alitoa taarifa ya uongo kwenye fomu aliyoijaza akidai kwamba alikuwa hatumii mihadarati kinyume cha sheria au alikuwa si mraibu wa madawa hayo ya kulevya.

Mnamo mwezi Septemba, alifikishwa kizimbani jimboni California akituhumiwa kutolipa kodi ya angalau dola milioni 1.4. Alikiri mashtaka hayo katika hatua iliyowashangaza wengi, saa kadhaa kabla majaji wa kusikiliza kesi yake kuanza kuchaguliwa.

Vyanzo: APE/AFP

Related Posts