SHIRIKISHO la Soka Barani Afrika (CAF) limemteua mwamuzi wa kati, Daniel Nii Ayi Laryea, raia wa Ghana kusimamia mchezo wa pili wa hatua ya makundi kati ya wenyeji MC Alger dhidi ya Yanga utakaopigwa Algeria Desemba 7, kwenye Uwanja wa du 5 Juillet.
Laryea aliyeanza kuoredheshwa kuwa mwamuzi wa kimataifa wa FIFA tangu mwaka 2014, amekuwa mwiba mkali zaidi kwa timu za ugenini kutokana na rekodi zake tangu achezeshe michuano hiyo, jambo ambalo Yanga inapaswa kujipanga ipasavyo kushinda.
Rekodi za mwamuzi huyo aliyezaliwa Septemba 11, 1987, zinaonyesha amechezesha mechi 24 za kimataifa, ambapo timu za nyumbani zimeshinda 13, sare nane huku za ugenini zikishinda mitatu, wakati kadi za njano ametoa 80 na nyekundu tatu.
Mwamuzi huyo anakumbukwa pia na kikosi hicho cha Jangwani kwani aliwahi kuichezesha Yanga ilipochapwa ugenini mabao 4-0, dhidi ya USM Alger ya Algeria zikiwa kundi ‘D’ la Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi, mechi iliyopigwa Mei 6, 2018.
Katika kundi hilo USM Alger ilimaliza kinara na pointi 11, ikifuatiwa na Rayon Sports ya Rwanda iliyokuwa na pointi tisa huku Gor Mahia ya Kenya ikishika nafasi ya tatu na pointi nane wakati Yanga iliburuza mkia baada ya kukusanya pointi nne tu.
Pia aliichezesha Simba katika michezo miwili akianza na ule wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi ambapo timu hiyo ilichapwa ugenini mabao 2-0, dhidi ya RS Berkane kutoka Morocco, mechi ya kundi ‘D’ iliyopigwa Februari 27, 2022.
Mechi nyingine aliyoichezesha ni ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi ambao Simba ilishinda mabao 6-0, dhidi ya Jwaneng Galaxy kutoka Botswana, katika mchezo wa kundi ‘B’ uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Machi 2, 2024.
Yanga iliyopo kundi ‘A’ la michuano hiyo inaingia katika mchezo huo ikihitaji ushindi ili kujiwekea mazingira mazuri ya kufufua matumaini ya kusonga mbele baada ya mechi ya kwanza nyumbani kuchapwa kwa mabao 2-0 na Al Hilal ya Sudan.
Timu hiyo ya Jangwani chini ya kocha mpya Mjerumani, Sead Ramovic aliyechukua nafasi ya Miguel Gamondi, ina kazi kubwa ya kufanya katika kundi hilo lenye pia TP Mazembe ya DR Congo ili kufika au kuivuka rekodi ya kuishia robo fainali msimu uliopita.
Yanga ilifika makundi ya michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo kwa rekodi ya aina yake baada ya kufuzu kwa jumla ya mabao 17-0, kwani katika mechi zake za raundi ya awali iliiondosha Vital’O kutoka Burundi kwa jumla ya mabao 10-0.
Baada ya Yanga kufuzu hatua ya hiyo ya awali, ikakutana na CBE SA ya Ethiopia ambapo mechi yake ya kwanza ikiwa ugenini ilishinda bao 1-0, huku mchezo wa marudiano uliopigwa Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar ikashinda mabao 6-0.
Kwa upande wa MC Alger iliyoanzia pia hatua ya awali ilianza kwa kuitoa Watanga FC ya Liberia kwa jumla ya mabao 4-0, baada ya kushinda 2-0 nyumbani na ugenini kisha baada ya hapo ikaitoa US Monastir kutoka Tunisia kwa jumla ya mabao 2-1.
MC Alger anayoichezea aliyekuwa nyota wa Azam FC, Kipre Junior, katika Ligi Kuu ya Algeria ‘Ligue 1’, imecheza mechi tisa ambapo kati ya hizo imeshinda nne, sare nne na kupoteza moja tu, ikishika nafasi ya tatu kwa pointi zake 16.
Kikosi hicho kipo pointi sawa na USM Alger iliyopo nafasi ya pili ila zimetofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa tu nyuma ya vinara CS Constantine inayoongoza na pointi 18, ingawa imecheza michezo 10 tofauti na wenzao waliocheza tisa.
Katika michezo hiyo tisa, kikosi hicho kimekuwa hakina uwiano mzuri wa kufunga kwani kimefunga mabao manane na kuruhusu sita.