USHINDI wa mechi mbili mfululizo katika Ligi Kuu Bara umempa ahueni kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, ambaye sasa ana matumaini makubwa ya kuendeleza rekodi nzuri kwenye michezo ijayo.
Ally anaamini timu yake inaweza kufanikisha matokeo mazuri, hususani katika michezo mitatu mfululizo inayowakabili nyumbani, ukiwamo mmoja wa Kombe la FA dhidi ya Igunga United.
Baada ya kupoteza mechi mbili ngumu, moja dhidi ya bingwa mtetezi Yanga (2-0) na nyingine dhidi ya Dodoma Jiji (1-0) ugenini, JKT Tanzania imejibu mapigo kwa ushindi wa michezo miwili dhidi ya Tanzania Prisons na Fountain Gate, yote kwa ushindi wa 1-0. Matokeo hayo yameipa timu hiyo jumla ya pointi 16, ikiwa sawa na Mashujaa iliyopo nafasi ya saba, huku JKT ikiwa katika nafasi ya nane.
Kocha Ally alizungumzia hali ya timu yake na matarajio yao katika michezo ijayo akisema: “Kujipanga upya baada ya kupoteza dhidi ya Yanga na Dodoma Jiji lilikuwa jambo muhimu kwetu. Vijana walionyesha dhamira kubwa na umoja wa kupambana na sasa tumevuna pointi muhimu. Tuna mechi tatu mfululizo nyumbani, na tunataka kuhakikisha tunadumisha rekodi yetu ya kutokupoteza nyumbani,” alisema.
Rekodi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ni ya kipekee, wakiwa wamecheza mechi tano wakishinda tatu dhidi ya Tanzania Prisons (1-0), Tabora (4-2) na Coastal Union (2-1), huku wakitoka sare dhidi ya KMC na Azam FC.
Ally alitambua umuhimu wa uwanja wa nyumbani na sapoti ya mashabiki wao.
“Nyumbani kwetu ni ngome imara. Mashabiki wetu wanatupa nguvu ya ziada na tunataka kuhakikisha tunaendelea kuwapa furaha. Hii ni nafasi yetu ya kusonga mbele kwenye ligi na pia katika Kombe la FA.”