NEEMA Olomi ameonyesha kiwango bora kabisa katika michuano ya gofu ya ubingwa wa Afrika iliyomalizka mwishoni mwa wiki mjini Agadir, Morocco baada ya kushika nafasi ya saba kati ya zaidi ya wachezaji 60 kutoka mataifa 20 yaliyoshiriki michuano hii.
Alama alizopata pia ziliiwezesha Tanzania kushika nafasi ya tano ikiwa nyuma ya Uganda, Kenya, Afrika Kusini na mabingwa wapya, Morocco.
Olomi alianza mashimo 18 ya kwanza kwa kupiga mikwaju 81, lakini akacharuka siku ya pili kwa kupiga mikwaju 76 kabla ya kumaliza mashimo 18 ya mwisho na mikwaju 79. Alipiga jumla ya mikwaju 236 ambayo ni matokeo ya saba kwa ubora kwa wachezaji binafsi.
Msichana wa miaka 16, Sofia Cherif Essakali kutoka Morocco ndiye aliyeshinda kwa kuwa na alama bora kwa wachezaji binafsi baada ya kupiga jumla ya mikwaju 204.
Alianza siku kwa mikwaju 69 na baadaye kuishangaza dunia kwa kupiga mikwaju 66 na kumaliza mashindano na mikwaju 69.
Mikwaju 66 ya siku ya pili ndiyo iliyoibeba Morocco dhidi ya mabingwa wa kihistoria Afrika Kusini, kwani hata mabingwa wa dunia ni nadra sana kupiga mikwaju 66.
Akiwa na jumla ya mikwaju 210, Kesha Louw wa Afrika Kusini alimaliza katika nafasi ya pil mbele ya mwenzake Lisa Lisa Coetzer aliyepiga mikwaju 217.
Nafasi ya nne ilitwaliwa na Mkenya Biana Ngecu aliyepiga jumla ya mikwaju 220 akifuatiwa na Mkenya mwenzake Mercy Nyamchama na Rim Imni wenye 223.
Nafasi ya sita ilichukuliwa tena na Mkenya Naomi Wafula aliyepiga mikwaju 226 kabla ya Mtanzania Neema Olomi kushika nafasi ya saba akifungana na Mganda Peace Kabasweka baada ya wote kupiga mikwaju 236.
Kitimu, Tanzania ilimaliza katika nafasi ya tano ikiwa nyuma ya Uganda kwa mkwaju mmoja baada ya kupiga jumla ya mikwaju 476.
Tanzania ilianza siku kwa kupiga jumla ya mikwaju 161 na ikajiimarisha siku ya pili na mikwaju 157 kabla ya kumaliza mashimo 18 ya mwisho na jumla ya mikwaju 158.
Washindi wa jumla Morroco, walipiga jumla ya mikwaju 425 wakifutiwa na Afrika Kusini walipiga jumla ya mikwaju 427.
Wakimaliza na jumla ya mikwaju 439, Kenya walimaliza katika na nafasi ya tatu wakati Uganda, waliopiga jumla ya mikwaju 475, walishika nafasi ya nne wakiwa mbele ya Tanzania kwa mkwaju mmoja.
Nafasi ya sita ilichukuliwa na Zimbabwe walioandika mikwaju 481 wakati Misri walishika nafasi ya saba wakiwa na jumla ya mikwaju 509.
Nafasi ya nane ilichukuliwa na Botswana waliopata alama 512, Tunisia wakawa wa tisa baada ya kupiga mikwaju 515.
Nchi nyingine ni Mauritius nafasi ya 10 kwa mikwaju 532.