Mwalimu Wenseslaus kutembea umbali wa zaidi ya Kilomita 800 kwa baiskeli kushiriki Sherehe za maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania

Mwalimu Wenseslaus Lugaya(34) anatarajajia kutumia Siku Nane kutembea umbali wa zaidi ya Kilomita 800 kwa baiskeli kutoka Mkoani Kigoma hadi Dodoma kushiriki Sherehe za maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania bara ifikapo Desemba 9,2024 sambamba na kutumia safari hiyo kwa ajili ya kutangaza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kutekeleza miradi ya Maendeleo na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa wananchi.

Mwal. Lugaya amekutana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe.Thobias Andengenye kwa ajili ya kumuaga na kukabidhiwa Bendera ya Tanzania na kusisitiza kuwa, jamii inapaswa kutambua kazi nzuri zinazofanywa na serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia jumbe mbalimbali ili kuongeza utayari katika kujitolea kuchangia nguvu katika ujenzi wa Taifa.

Lugaya maarufu kama Gadafi, ambae pia ni Mwalimu Mkuu katika Shule ya Msingi Junga iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu, ameanza Safari hiyo Jana Desemba Mosi ,2024 katika Manispaa ya Kigoma Ujiji akitokea Wilayani Kasulu kwa baiskeli huku akitarajia kuwasili mkoani Dodoma Desemba 8, 2024 kupitia Barabara ya Uvinza, Tabora, Itigi hadi jijini Dodoma.

Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amempongeza Mwalimu Lugaya kwa dhamira yake pamoja na kuahidi kumuunga mkono katika mchakato mzima wa safari hiyo na kumkabidhi bendera ya Tanzania na Pesa ya kujikumu,Pamoja na hayo Andengenye ametoa wito kwa vijana mkoani hapa kujenga tabia ya uzalendo kwa kutambua kazi nzuri zinazofanywa na serikali pamoja na kuwa na utayari katika kushiriki shughuli za Maendeleo.

Ikumbukwe hii sio mara ya kwanza kwa baadhi ya wakazi wa Kigoma kufunga safari kutoka kigoma kwenda Dodoma hadi Dar hasa kwa miguu kwa malengo mbalimbali ikwepo Shabiki wa Yanga aliyetembea kwa miguu kutoka kigoma hadi Dar es Salaam mwaka 2021 na wengine tofauti fofauti walifunga safari kwa lengo la kumpongeza Rais wa Tanzania.

Related Posts