Tarehe kama ya jana, Disemba Mosi, mwaka 2006, Mrisho Khalfan Ngassa aliifungia Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) bao moja katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Djibouti, kwenye mashindano ya CECAFA Senior Challenge Cup, yaliyofanyika Ethiopia.
Ngassa alifunga bao hili akiwa na miaka 17, miezi 6 na siku 26, kutokana na taarifa zake rasmi kwamba alizaliwa Mei 5, 1989,
Bao hilo linahesabika kama bao la kwanza kwa Mrisho Ngassa kwenye timu ya taifa, katika mabao yake 25.
Kwa mabao hayo 25, Mrisho Khalfan Ngassa anatajwa kama mfungaji bora wa muda wote wa Taifa Stars.
Lakini lile bao Ngassa hakuifungia Taifa Stars bali Kilimanjaro Stars, kwa nini lihesabiwe kwenye mabao yake ya Taifa Stars?
Hapa ndipo kwenye msingi wa hoja yangu.
Taifa Stars ni timu ya taifa ya Tanzania inayoundwa na wachezaji kutoka pande zote mbili za muungano, bara na visiwani, na hushiriki mashindano ya CAF na FIFA kama timu rasmi ya ya taifa ya Tanzania.
Kilimanjaro Stars ni timu inayoundwa na wachezaji wa bara pekee, na hushiriki mashindano ya CECAFA pekee, kama Tanzania Bara, sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika mabao yake 25 yanayohesabiwa kama mabao rasmi ya Ngassa kwa Taifa Stars, mabao 16 ameyafunga kwenye CECAFA.
Katika mabao yao 16 ya CECAFA, moja amelifunga dhidi ya Zanzibar ambayo ni sehemu ya Tanzania…unaona vituko vyake?
Yaani mfungaji bora wa muda wote wa Tanzania anahesabiwa magoli ambayo aliifunga Tanzania.Kuna kitu hakiko sawa!
Katika rekodi hizi, bao lake dhidi ya Ivory Coast, 25 Februari 2009, kwenye mashindano ya kwanza kabisa ya CHAN yaliyofanyika nchini Ivory Coast, halimo.
Na hii ni kwa sababu mashindano yale hayakuwa rasmi wakati ule, tofauti na sasa ambapo FIFA wanayatambua.
Lakini ni afadhali lingeorodheshwa bao lile ambalo ni la timu ya taifa ya Tanzania inayoundwa na wachezaji kutoka pande zote za muungano, kuliko haya ya Kilimanjaro Stars.
Mgawanyiko wa mabao ya Mrisho Ngassa kama yanavyosomeka kwenye tovuti ya TFF.
Namba Mechi Tarehe Mashindano Bao la mchezo
1 Kilimanjaro Stars 3-0 Djibout 1/12/2006 CECAFA (1)
2 Taifa Stars 3-1 Cape Verde 11/10/2008 Kombe la Dunia 2010 (3)
3 Kilimanjaro Stars 2-0 Rwanda 1/7/2009 CECAFA (1)
4 Kilimanjaro Stars 3-2 Burundi 13/1/2009 CECAFA (1)
5 Kilimanjaro Stars 1-0 Zanzibar 1/12/2009 CECAFA (1)
6 Kilimanjaro Stars 1-0 Burundi 4/12/2009 CECAFA (1)
7, 8 & 9Kilimanjaro Stars 4-0 Eritrea 8/12/2009 CECAFA (3)
10 Taifa Stars 3-2 Uganda 3/3/2010 Kirafiki (1)
11 Taifa Stars 1-1 Rwanda 1/5/2010 Kirafiki (1)
12 Taifa Stars 1-1 Kenya 11/8/2010 Kirafiki (1)
13 Taifa Stars 1-0 Palestina 9/2/2011 Kirafiki (1)
14 Chad 0-1 Taifa Stars 11/11/2011 Kufuzu Kombe la Dunia 2014 (1)
15 Kilimanjaro Stars 1-3 Uganda 8/11/2011 CECAFA (1)
16 Taifa Stars 3-3 Botswana 15/12/2012 Kirafiki (1)
17, 18, 19, 20, 21 Kilimanjaro Stars 5-0 Somalia 1/12/2012 CECAFA (5)
22 Taifa Stars 1-0 Zambia 22/12/2012 Kirafiki (1)
23 & 24 Kilimanjaro Stars 2-2 Uganda 7/12/2013 CECAFA (2)
25 Taifa Stars 1-1 Malawi 29/3/2015 Kirafiki (1)
Kwa kifupi Mrisho Ngassa amefunga mabao mengi zaidi kwenye CECAFA na mechi za kirafiki. Hizi za kirafiki ni zile rasmi za kwenye kalenda ya FIFA, kwa hiyo zinastahili kuwemo kwenye rekodi rasmi, lakini zile za CECAFA, hapana.
CECAFA siyo mashindano yanayoihusisha Taifa Stars, kwa hiyo haipaswi Ngassa kuhesabiwa mfungaji bora wa muda wote wa Taifa Stars kwa mabao ya CECAFA.
Ifuatayo ni orodha ya tano bora inayostahili ya wafungaji bora wa muda wote wa Taifa Stars, bila kuhusisha mabao ya.
Jina Mabao Taifa Stars Mabao Kilimanjaro Stars
Saimon Msuva 20 3
Mbwana Samatta 20 2
John Bocco 9 7
Mrisho Ngassa 9 16
Nteze John 7 5
Kwa tafsiri rahisi ni kwamba Saimon Msuva na Mbwana Samatta ndiyo wafungaji bora wa muda wote wa Taifa Stars kwa mabao yao 20 kila mmoja.
Mrisho Ngassa analingana na John Bocco ambao wote wana mabao 9 kila mmoja.