Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali wa kitaifa wamefika katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam kuhudhuria misa maalumu ya kumuaga aliyekuwa mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika Dk Faustine Ndugulile.
Misa hiyo itakayoendeshwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Lameck Stephano Msomba, imehudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu serikalini, wakiwemo mawaziri na wabunge na Rais Samia Suluhu Hassan.
Wengine waliopo ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Mkurugenzi wa WHO Afrika Dk Moeti, Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi.
Miongoni mwa waombolezaji waliohudhuria misa hiyo leo Jumatatu, Desemba 2, 2024 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam wamemzungumzia Ndugulile kama kiongozi wa mfano na mwenye uthubutu.
“Sisi wananchi wa Kigamboni tutamkumbuka sana, alikuwa akitupigania. Tulishakubali kwamba anaondoka kwenda WHO, lakini hiki kilichotokea kimetuumiza zaidi,” amesema Lazaro Japhet, mkazi wa Kigamboni.
Mwili wa Ndugulile utawasili eneo hilo baada ya viongozi wote kuwasili na itafanyika misa takatifu, ikifuatiwa na wasifu wa marehemu na salamu kutoka kwa viongozi mbalimbali.
Pia kutakua na salamu za pole kutoka kwa viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, kabla ya Rais Samia kuwaongoza viongozi na wageni mbalimbali kutoa heshima zao za mwisho.
Saa 8:30 mchana mwili wa Dk Ndugulile utaelekea nyumbani kwake Kigamboni kwa ajili ya taratibu za mazishi yatakayofanyika kesho Jumanne katika makaburi ya Mwongozo.
Kifo cha Dk Ndugulile kimewaacha wengi wakitafakari juu ya urithi ambao angeendelea kuujenga kama Mkurugenzi wa Kanda wa WHO Kanda Afrika.
Alikuwa ameainisha vipaumbele kadhaa kwa kipindi chake cha uongozi, ikiwemo kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, kuimarisha maandalizi kwa dharura za kiafya na kuendeleza ushirikiano wa kina na taasisi mbalimbali za afya.
Alipanga pia kuleta ushiriki zaidi wa mabunge ya Afrika katika shughuli za WHO, mtazamo wa kipekee aliokuwa akinuia kuingiza katika uongozi wake.
Katika kampeni yake ya kugombea nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda ya WHO Afrika, alisisitiza umuhimu wa uongozi thabiti na wa maono katika sekta ya afya barani Afrika.
Alisema nchi za Afrika zinahitaji viongozi wanaochanganya uwezo wa kitaaluma na uzoefu wa kisasa, ili kukabiliana na changamoto kubwa za kiafya zinazolikumba bara hili.
“Ninaamini Afrika inastahili kiongozi anayeweza kuendesha sekta ya afya mbele, hasa tunapokaribia hatua za mwisho za Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs),” alisema Dk Ndugulile wakati wa kampeni yake.
Pia alikiri ushindani mkubwa aliokutana nao kutoka kwa wagombea waliokuwa na uzoefu wa muda mrefu, lakini alibaki na imani na uwezo wake wa kufanikisha kipindi chake cha miaka mitano, ambacho kingaweza kuongezwa kulingana na utendaji.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali