Unguja. Licha ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)kueleza kuwa, haijafanya tathmini kuhusu wananchi wanaotumia nishati mbadala, imesema matumizi ya gesi yameongezeka kisiwani humo ikiwa ni ishara ya kuachana na matumizi ya nishati chafu.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harusi Said Suleiman matumizi ya gesi yameongezeka kutoka ujazo wa kilogramu 7,200,126 mwaka 2022 hadi kufikia ujazo wa kilogramu 9,673, 170 mwaka 2023.
Harusi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Desemba 2, 2024, katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi wakati akijibu swali la mwakilishi, Mwantatu Mbaraka Khamis wa nafasi za wanawake aliyetaka kujua tathmini ya matumizi ya nishati mbadala kwa lengo la kuhifadhi mazingira.
“Bado wizara haijafanya tathmini kujua idadi halisi ya watu wanaotumia nishati safi ya kupikia, licha ya juhudi mbalimbali zinazochukuliwa kwa kutoa mitungi ya gesi na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala,” amesema Harusi.
Amesema kwa kuzingatia juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ikiwamo kugawa mitungi ya gesi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama, matarajio yao ni kuwa ifikapo mwaka 2025 asilimia ya watumiaji itakuwa imeongezeka zaidi.
“Tunatarajia ifikapo mwaka 2025 asilimia kubwa ya watu watakuwa wanatumia nishati safi ya kupikia,” amesema.