HATIMAYE matajiri wa Chamazi, Azam FC wamerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya miezi tisa na siku 26 (sawa na siku 300) kufuatia ushindi wa mabao 3-1 ambao waliupata juzi, Jumapili kwenye Uwanja wa Jamhuri dhidi ya wenyeji wao, Dodoma jiji.
Mara ya mwisho kwa Azam kuwa kileleni mwa msimo wa Ligi Kuu Bara ilikuwa Februari 5, mwaka huu msimu uliopita wa 2023/24 baada kufikisha pointi 31 huku wakiwa mbele kwa mchezo mmoja dhidi ya Yanga ambao walikuwa na pointi 31 na miwili dhidi ya Simba ambao walikuwa na pointi 26.
Wakati huo wakiwa chini ya kocha Msenegal, Youssouph Dabo, walikuwa wakiongoza msimamo huo kwa tofauti ya mabao kabla ya kushushwa na Yanga ambao walikwea kileleni baada ya kuitandika Dodoma Jiji bao 1-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex na kufikisha pointi 34.
Wale ambao waligeuka ngazi kwa Yanga kukwea kileleni kwa kuishusha Azam msimu uliopita ndio hao hao ambao msimu huu wamekiona chamoto mbele ya matajiri hao kwa kufungwa mabao 3-1, mabao ya Azam kwenye mchezo huo, yalifungwa na Nassor Saadun, Feisal Salum na Dickson Mhilu ambaye alijifunga. Bao la Dodoma, Yannick Bangala wa Azam alijifunga.
Kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita ambapo waliongoza ligi huku Simba na Yanga wakiwa nyuma, ndivyo ilivyo hata msimu huu, Azam imefikisha pointi 30 ndani ya michezo 13 huku Simba yenye pointi 28 na Yanga yenye 27 zikiwa nyuma kwa michezo miwili.
Ushindi dhidi ya Dodoma Jiji, umeifanya Azam kushinda mchezo wa sababu mfululizo msimu huu katika ligi, jambo ambalo linamfanya kocha wa kikosi hicho, Rachid Taoussi kuwa na matumaini ya kufanya makubwa zaidi.
“Kwanza kabisa natoa pongezi kwa wachezaji wangu kwa kazi nzuri na kubwa ambayo wameifanya, tulikuwa na mchezo mgumu ambao tumeushinda, haikuwa rahisi kutoka nyuma, ni furaha iliyoje kwetu kuongoza ligi, kilichopo ni kuendelea kupambana na kusalia nafasi hii,” alisema kocha huyo.
Kwa upande wake, Saadun ambaye amefikisha mabao manne msimu huu, alisema; “Natamani kuona tukitwaa ubingwa wa ligi, najua ni kazi ngumu na kubwa hivyo tunatakiwa kuendelea kufanya vizuri mchezo baada ya mchezo.”
Katika michezo 13 waliyocheza ya ligi msimu huu, Azam imefunga mabao 19 ni sawa na wastani wa 1.4, msimu uliopita wanaonekana walikuwa moto wa kuotea mbali zaidi katika uchekaji na nyavu kwani kipindi kama hiki walifunga mabao 35 hivyo walikuwa na wastani wa kufunga mabao 2.5.