MWENYE ULEMAVU ZAIDI YA 300 KONDOA KUJENGEWA UWEZO MASUALA YA UONGOZI

Na Paul Mabeja, DODOMA
ZAIDI ya Sh. milioni 40 zimetolewa na Shirika lisilo la kiserikali la Abilis Foundation kwa ajili ya kutekeleza mradi wa mwaka mmoja wa kuwajengea uwezo wanawake vijana wenye ulemavu kwenye masuala ya uongozi wilayani Kondoa mkoani hapa ili kukuza demokrasia nchini.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa na shirika la kuhudumia watu wenye ulemavu la mkoani hapa la Foundation For Disabilities Hope (FDH) ambapo zaidi ya watu wenye ulemavu 300 watarajiwa kufikiwa.
Mkurugenzi wa FDH, Michael Salali alisema hayo jana jijini hapa wakati akitambulisha mradi huo kwa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule kwa ajili ya utekelezaji wake.
Alisema lengo la mradi huo ni kuwajengea uwezo wanawake vijana walemavu kukamata fursa za uongozi katika jamii yao na kuondokana na tabia ya kujinyanyapaa wenyewe.
“Mafunzo tutakayotoa yatasaidia kundi hili kuondokana na dhana potofu ya walemavu kujichukulia kuwa wao hawezi kuwa viongozi badala yake wajitokeze kwa wingi kukamata fursa zote za uongozi zinazojitokeza mbele yao”alisema
Salali, alisema mradi huo ambao utatekelezwa katika wilaya ya Kondoa ni wa mwaka mmoja na fedha za mradi huo zimetolewa na Shirika la Abilis Foundation ambalo makao yake makuu yapo nchini Finland.
“Mradi huu wa mwaka mmoja sisi FDH tunakwenda kutekeleza lakini fedha za ufadhili ni kutoka Abilis Foundation shirika lenye makao makuu yake nchini Finland lakini hapa nchini ofisi zao zipo jijini Arusha”alisema Salali
Aidha, alisema mradi huo unakwenda kugusa makundi ya yote ya watu wenye ulemavu kwa ajili ya kuwajengea uwezo kwenye masuala ya uongozi na kukuza demokrasia pamoja na ujasiriamali.
“Leo tumekuwa na kikao na viongozi kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dodoma ambao ni wajumbe wa CHMT, lengo likiwa kwanza kuutambulisha mradi lakini pia uelewa kwasababu serikali na sisi kama wadau tunafanya kazi kwa pamoja hivyo hatuwezi kwenda kutekeleza mradi kama huu bila serikali kuufahamu na kutoa ushirikiano wake.
“Tunashukuru uongozi wa mkuu wa mkoa wa Dodoma kwa ushirikiano tuliopatiwa pamoja na watendaji wake kutoa ushirikiano kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi huu wa mwaka mmoja”alisema
Alisema, wanaahidi kwenda kutekeleza kile ambacho kimekusudiwa kwenye mradi huo na siyo vinginevyo ili kupata matokeo chanya na jamii ya watu wenye ulemavu iwe na uelewa wa kutosha na kuchagamkia fursa mbalimbali za uongozi.
Kadhalika, alisema wanahitaji kuona watu wenye ulemavu wanakamata fursa mbalimbali za kiungozi kwenye maeneo mengi nchini na kujenga msingi imara kwa kundi hilo.
“Kwanza mradi huu tunatarajia kuwafikia moja kwa moja watu 300 kwenye Kata ya Kilimani, Chemchem na Bolisa lakini pia makundi mengine katika jamii kupitia uhamasishaji wa vipindi vya redio na mikutano mbalimbali tutakayoifanya kwenye halmashauri ya Kondoa”alisema

Related Posts