ITAKUWAJE? Ndilo swali linalogonga vichwa vya mashabiki wa soka nchini kuhusu kukosekana kwa mshambuliaji wa Azam FC Mzimbambwe Prince Dube katika mechi ya leo ambayo wakali hao wa Chamazi watakuwa wenyeji uwanja wa Benjamin Mkapa kuikaribisha Simba ambayo Dube ameifunga katika mechi nne zilizopita mfululizo kabla ya kujiweka kando na timu hiyo.
Mgongano wa maslahi na mambo ya kimkataba yaliyopelekea Dube kukaa kando na timu hiyo kuanzia katikati ya mwezi Machi mwaka huu ni sababu kuu zitakazoifanya Azam kumkosa Straika huyo aliyeikoa timu hiyo kuepuka kipigo au sare katika mechi tatu za ligi zilizopita dhidi ya Simba kwa kufunga mabao yaliyowaondolea aibu wakali hao wa Chamazi.
Straika huyo alianza kuifunga Simba kwenye mechi ya ligi msimu wa 2022/2023 katika mechi zote mbili akianza kwenye mchezo wa duru ya kwanza ambapo Azam ilishinda bao 1-0, lililopachikwa na Dube dakika ya 35 ya mechi hiyo iliyopigwa Oktoba 27, 2022.
Mzimbabwe huyo aliifunga Simba tena kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa msimu huo iliyopigwa Februari 21, 2023 akipachika bao dakika ya pili kabla ya Kibu Denis kuisawazishia Simba dakika ya 90 na mechi kumalizika kwa sare ya mabao 1-1.
Dube hakupoa mbele ya kwani Mei 7, mwaka jana timu hizo zilikutana kwenye nusu fainali ya FA na Dube kuifungia Azam bao la ushindi dakika ya 75 katika mchezo ambao Azam ilianza kwa kufunga bao dakika ya 22 kupitia kwa Lusajo Mwaikenda kisha Sadio Kanoute kuisawazishia Simba dakika ya 28 kabla ya Dube kufunga bao hilo lililofanya mechi kuisha 2-1 na Azam kutinga fainali.
Wakati Simba ikijaribu kumsahau Dube, msimu huu katika mechi ya mzunguko wa kwanza aliwakumbusha tena uwepo wake kwa kuifungia Azam bao la kuongoza dakika ya 14 kabla ya Simba kusawazisha dakika ya 90 kupitia kwa Clatous Chama na mechi hiyo iliyopigwa uwanja wa CCM Kirumba Mwanza Februari 9, mwaka huu kumalizika kwa sare ya mabao 1-1.
Baada ya Dube kujiengua kikosini Azam, Simba ilipata ushindi dhidi ya timu hiyo ikiwa ni ule wa bao 1-0 ilioupata kwenye mechi ya fainali ya Ligi ya Muungano likifungwa na kiungo Babacar Sarr. Je? Leo Azam itaweza kuifunga Simba bila Dube, tusubiri dakika 90 zitaamua.
Muda ni kuanzia saa 12:15 jioni ambapo mtanange huo utaanza. Ni mechi ya kukata na shoka katika Ligi Kuu Bara. Mechi inayojulikana kwa umaarufu wa jina la ‘Mzizima Dabi’.
Ni mechi dume haswa. Mechi iliyobeba matumaini ya timu zote mbili kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu ujao lakini pia ni mechi ya kuamua ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Mchezo huo unazikutanisha Azam na Simba ambazo zote zinawania ubingwa wa ligi ‘kwa mbali’ lakini kubwa zaidi ni nafasi ya pili baada ya Yanga kuzizidi kete timu hizo ambapo kabla ya mechi ya jana na Kagera Sugar ilikuwa ikiziacha kwa pointi nane hadi 11 Simba na Azam.
Iko hivi; Msimu huu Tanzania itaingiza klabu nne kwenye mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ambapo mbili zitaenda Ligi ya Mabingwa na nyingine mbili zitatinga Shirikisho.
Kwa namna kanuni zilivyo, timu zitakazotinga Ligi ya Mabingwa michuano ambayo ni mikubwa zaidi Afrika kwa ngazi ya klabu ni zile mbili zilizomaliza katika nafasi za juu huku Kombe la Shirikisho zikienda Bingwa wa Kombe la FA, na timu iliyoshika nafasi ya tatu lakini kama bingwa wa FA atakuwa kati ya timu tatu za juu kwenye ligi basi timu itakayoshika nafasi ya nne katika ligi itashiriki Kombe la Shirikisho.
Kwa mantiki hiyo Simba na Azam zinawania nafasi moja tu ya kushiriki Ligi ya Mabigwa Afrika baada ya Yanga kuwa na uhakika wa kutwaa ubingwa msimu huu na kukata tiketi ya kushiriki mashindano hayo kwa msimu ujao kutokana na muendelezo wake bora ikiwa imesaliwa na mechi nne. Hivyo basi matokeo ya mechi ya leo yana nafasi kubwa ya kuamua ni timu gani itamaliza katika nafasi ya pili na kuungana na Yanga kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ikumbukwe Simba imekuwa na rekodi bora ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwani imefanya hivyo katika misimu sita iliyopita mfululizo hivyo haitataka kupoteza rekodi hiyo iliyoijenga Afrika lakini pia Azam inataka kushiriki michuano hiyo kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo msimu wa 2014/2015 na kutolewa katika hatua ya awali kwa jumla ya mabao 3-2 na El Merrikh ya Sudan.
Hadi sasa Azam ina pointi 57 baada ya mechi 25 ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi huku Simba ikiwa nafasi ya tatu na pointi 53 ilizovuna kwenye mechi 24.
Azam inahitaji ushindi au sare ili kuendelea kuwa juu ya Simba huku Wekundu wa Msimbazi hao wakitaka ushindi pekee ili kuwa na matumaini ya kumaliza nafasi ya pili.
Kwa namna msimamo ulivyo hadi sasa Azam inaizidi Simba pointi nne ambazo kama itashinda mechi hii itakuwa imeizidi pointi saba licha ya kwamba Simba itakuwa na mchezo wa kiporo ambao hata ikishinda kisha timu zote mbili zikashinda mechi zote zilizobaki (baada ya hii), Azam itakuwa juu ya Simba kwa pointi nne.
Endapo Simba ikishinda mechi hii, sambamba na tano nyingine zitakazofuata itamaliza katika nafasi ya pili, juu ya Azam kwa tofauti ya pointi mbili lakini kama mchezo huu utamalizika kwa sare basi itakuwa msala kwa Simba kwani Azam itahitaji kushinda mechi zake sita zilizosalia ili kumaliza nafasi ya pili na kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao. Matokeo yoyote yatakayopatikana kwenye mechi hii yatakuwa yakiisukuma Yanga kwenye ubingwa.
Mara nyingi Azam na Simba zinapokutana imekuwa mechi ambayo ni nadra kumalizika bila nyavu kutikisika. Kwenye mechi 11 zilizopita za ligi baina ya timu hizi mbili, ni mchezo mmoja pekee uliomalizika bila bao (0-0), mechi nyingine 10 zimemalizika kwa nyavu kutikiswa yakiwa yamefungwa jumla ya mabao 26, Simba ikifunga mengi zaidi (15) na Azam ikifunga 11, huku mchezo uliozalisha mabao mengi ukiwa ule wa Machi 4, 2020 ambapo Simba ilishinda 3-2.
Katika mechi hizo 11 za ligi zilizopita, matokeo ya sare yalitawala lakini hata hivyo Simba iliongoza kwa kushinda ikiibuka na ushindi mara nne huku Azam ikishinda mechi moja tu na sita zilizosalia kumalizika kwa sare.
Azam ndiyo ina matokeo mazuri zaidi katika mechi zake tano za ligi zilizopita kwani imeshinda nne na kutoa sare moja huku Simba ikiwa imeshinda mbili, sare mbili na kupoteza moja katika mechi zake tano za ligi zilizopita.
Moja ya sehemu iliyoshikilia hatma ya mchezo huu ni makocha wa timu hizi mbili. Juma Mgunda na Seleman Matola wa Simba sambamba na Bruno Ferry na Youssoupha Dabo wa Azam ambao watakuwa watendaji wakuu kwenye mechi hii kutokea kwenye mabenchi la ufundi.
Mgunda aliyeanza kuinoa Simba Aprili 30 kwenye mechi ya ligi dhidi ya Namungo iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2 baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha mkuu wa chama hilo, Abdelhack Benchikha alisema ni mechi ngumu lakini timu yake imejipanga kufanya vizuri. “Tutawakosa baadhi ya nyota wetu wakiwemo, Chama (Clatous), Luis (Miquissone), Saido (Ntibanzokiza) lakini Simba ina wachezaji wengi na wote wapo hapa kucheza,” alisema Mgunda aliyewahi kuichezea na kuifundisha Coastal Union.
“Tutatumia wachezaji waliofiti na tunaamini wakijituma na kufuata vyema maelekezo basi tutashinda.”
Mgunda tangu ameichukua Simba ameibadili kiuchezaji na ametoa nafasi kwa wachezaji ambao awali nafasi yao ilikuwa finyu kikosini wakiwemo, Edwin Balua, Ladack Chasambi, Salehe Karabaka na Mzamiru Yassin ambao wamekuwa na matokeo chanya kwani katika mechi tatu ambazo kocha huyo kipenzi cha mashabiki ameiongoza Simba, imeshinda mbili na kutoa sare moja ikivuna pointi saba na kufunga mabao sita huku ikiruhusu mawili pekee.
Nyota wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella alimsifu Mgunda kwa kuibadili timu hiyo lakini alisema ushindani wa mchezo huu unachagizwa na nafasi zilizopo timu hizo na anaamini hautokuwa mchezo mwepesi kutokana na ubora wa Azam na mabadiliko ya Simba kiuchezaji tangu ujio wa Mgunda.
“Kocha, Juma Mgunda ameibadilisha sana Simba kiuchezaji kwa sababu unaona timu inacheza vizuri na kila mchezaji amempa nafasi ya kucheza ingawa hautokuwa mchezo mwepesi kwani Azam nayo imeonyesha ina wachezaji wanaoweza kuamua matokeo.”
Upande wa Ferry na Dabo ambao tangu wametua kikosini hapo mwishoni mwa msimu uliopita na kuanza kazi rasmi msimu huu wakiibadili Azam kiuchezaji wanatarajiwa kuwa na mtihani mkubwa mbele ya Simba iliyo chini ya Mgunda na Matola yenye mabadiliko makubwa.
Ferry alisema watahakikisha wanapambana ili kujiwekea mazingira mazuri ya nafasi ya pili huku akiainisha watalipa kisasi kutokana na matokeo ya mwisho walipofungwa bao 1-0, kwenye fainali ya Ligi ya Muungano.
“Unapocheza na Simba siku zote hauwezi kuwa mchezo mwepesi kwa sababu ya ubora wa wachezaji wakubwa ilionao ila hata sisi tunauhitaji wa kupata matokeo bora ili kuzidi kujiwekea mazingira mazuri ya kuendelea kushikilia juu zaidi,” alisema Ferry.
Katika mchezo huo Azam itawakosa Wachezaji majeruhi Ali Ahmada, Malickou Ndoye, Sospeter Bajana, Alassane Diao, Abdullah Idrissu, Franklin Navarro na mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Prince Dube mwenye matatizo na timu hiyo kuhusiana na suala la mkataba.
Eneo la kiungo la Simba leo huenda wakacheza baadhi kati ya Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute, Babacar Sarr, Mzamiru Yassin, Edwin Balua na Ladack Chasambi.
Simba imekuwa ikitumia eneo hilo katika kuanzisha mashambulizi, kujilinda na kufunga na kuzifanya timu pinzani kuwa na wakati mgumu kulidhibiti.
Ukiachana na eno hilo, pia mtu hatari kuchungwa kwa Simba ni mshambuliaji, Freddy Michael aliyetua kikosini hapo kwenye dirisha dogo la usajiri lililofungwa Januari 15 mwaka huu akiwa hadi sasa amefunga mabao matano kwenye ligi katika mechi 14 alizocheza.
Kwa upande wa Azam ambayo kwa sasa inacheza bila mshambuliaji wa kati asilia baada ya Dube kuondoka, Navarro na Diao kuwa majeraha, viungo ndio mhimili mkuu wa timu hiyo katika kufunga na kutengeneza nafasi.
Djibril Sylla, Kipre Jr, Abdul Sopu, Ayoub Lyanga, James Akaminko, Adolf Mtegesi, Yahya Zayd na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye ni kinara wa mabao kikosini hapo akifunga mara 15 kwenye ligi, wanatarajiwa kuwepo kwenye kikosi cha leo.
Nyota wa zamani wa Azam na Kagera Sugar Philip Alando alisema mchezo huo utakuwa mgumu kwa timu zote mbili kutokana na mahitaji yao ya kuwania nafasi mbili za juu huku akiweka wazi atakayecheza kwa nidhamu atakuwa na nafasi ya kushinda sambamba na kulitaja eneo la kiungo kuamua mechi hiyo.
“Ni mchezo ambao naona utaamuliwa zaidi katikati ya uwanja kwa sababu ya ubora wa timu zote mbili kwenye maeneo hayo, kwangu itakuwa mechi ya kuvutia hasa kutokana na ushindani uliopo na pia matokeo mazuri ambayo timu hizo mbili zimetoka kuyapata katika mechi zilizopita,” alisema Alando aliyekuwa mshambuliaji hatari katika wakati wake.
Mwamuzi wa pembeni ni kutoka Sudan. Ibrahim Abdallah atakayeshika kibendera kama mwamuzi msaidizi namba moja huku msaidizi namba mbili akiwa Mohamed Mkono kutoka Tanga huku Mwanadada Amina Kyando kutoka Morogoro akiwa mwamuzi wa nne na katikati ya uwanja mwamuzi mkuu atakuwa Ahmed Arajiga kutokea Manyara ambaye mara nyingi amekuwa akichezesha mechi kubwa.