Mahakama Kuu yatupa maombi ya Mdude, aendelea kushikiliwa

Mbeya. Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya imetupilia mbali maombi ya mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mdude Nyagali, aliyekuwa akiomba kufikishwa mahakamani au kuachiwa huru tangu akamatwe na polisi Novemba 22, mwaka huu.

Maombi hayo yaliwasilishwa na mawakili wa kujitegemea, Boniface Mwabukusi na Philipo Mwakilima, mbele ya Jaji Mussa Pomo.

Shauri hilo lilianza kusikilizwa Novemba 28, 2024, lakini liliahirishwa hadi Novemba 29 kwa sababu Mahakama ilikuwa ikisikiliza na kutoa uamuzi katika kesi za mauaji.

Leo Jumatatu, Desemba 2, 2024, Mahakama hiyo imetoa uamuzi kwa kutupilia mbali maombi hayo, ikitaja sababu udhaifu wa kiapo kinzani cha waleta maombi, hususan kifungu cha 5 na 12.

Jaji Mussa Pomo amesema kiapo hicho hakikuonyesha ushahidi wa moja kwa moja kuthibitisha Mdude amejeruhiwa au kushikiliwa kinyume cha sheria.

Aidha, Jaji Pomo amebainisha kuwa wakili, Philip Mwakilima hakutoa ushahidi wa kushuhudia moja kwa moja tukio la Mdude kupigwa au kuteswa na kwamba hoja zilizotolewa katika kiapo kinzani ni uelewa wa mleta maombi, badala ya ushahidi thabiti.

Hatua za rufaa
Hata hivyo, Jaji Pomo ameushauri upande wa waleta maombi kukata rufaa, endapo hawajaridhika na uamuzi huo wa Mahakama.

Mwenendo wa shauri
Mawakili wa mleta maombi waliwasilisha ombi hilo Novemba 26, mwaka huu, wakitaka Mahakama iagize Mdude kufikishwa mahakamani au kuachiwa huru.

Ombi hilo lilihusisha madai kuwa Mdude anashikiliwa kinyume cha sheria na Jeshi la Polisi.

Shauri hilo namba 33247/2024, lilisimamiwa na mawakili wa Serikali, Lodgard Eliaman na Dominic Mushi, huku upande wa waleta maombi ukiwakilishwa na Boniface Mwabukusi na Philip Mwakilima.

Akizungumza baada ya shauri hilo kutupiliwa mbali, Wakili Mwabukusi amesema hawakubaliani na uamuzi wa Mahakama na hivyo watajadiliana kuona hatua bora za kuchukua.

“Kwa sababu tunaamini Mdude Nyagali alipigwa na anashikiliwa kinyume cha sheria, tungeomba Mahakama itende haki. Ikiwa ana kosa, basi wakati shauri linaendelea angefikishwa mahakamani,” amesema Mwabukusi.

Kwa upande wake, Wailolo Mwakilima amesema kwa sasa hawezi kusema chochote kwa sababu hakuna Mtanzania ambaye hakuona tukio la kushambuliwa kwa mwanaharakati huyo.

“Watanzania wana macho, waliona. Ndio maana hoja yetu ilikuwa kwamba, kama ana kosa linalowalazimu kumshikilia, wangemfikisha mahakamani au kumwachia huru,” amesema.

Awali, Novemba 22 mwaka huu, kada huyo wa Chadema alikuwa miongoni mwa viongozi waliokamatwa na Polisi wa Mkoa wa Songwe, akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi (Sugu), ambao waliachiwa kwa dhamana, huku Mdude akiendelea kushikiliwa.

Related Posts