Yas yataja sababu kubadili jina, vipaumbele

Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mpito wa Kampuni ya Yas Tanzania, Jerome Albou ametaja sababu zilizoifanya kampuni hiyo kubadili jina kutoka Tigo.

Albou amesema lengo lao kuu ni kutaka kuboresha huduma za mtandao ili ziwe za kisasa zaidi huku zikimgusa kila mtu.

Ofisa huyo amesema hayo leo Jumatatu Desemba 2, 2024 alipofanya mazungumzo maalumu yaliyoongozwa na Kaimu Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited, Mpoki Thomson.

Amesema dhumuni lingine la kampuni hiyo ni kutaka kuwafikia watu wengi zaidi popote pale walipo nchini hususani vijana.

Albou amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokuwa kiteknolojia kama ilivyo duniani, hivyo wameamua kuja kidijitali zaidi.

Albou amesema hatua hiyo imekuja na mabadiliko mapya yanayojikita kwenye mchango wa kampuni hiyo ya mawasiliano nchini.

Amesema Yas ni mtandao unaomgusa karibu kila Mtanzania hususani vijana, hivyo wataendelea kuboresha zaidi huduma wanazozitoa nchini kwa zaidi ya miaka 14 sasa.

Amezitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na ya Tigo Pesa, Tigo Rusha na nyingine nyingi.

“Tumekuwa tukiongoza katika ubunifu, tutaendelea kufanya hivyo, watu watarajie mambo mazuri. Kila siku tunaangalia mteja anataka nini nasi tunaboresha zaidi na zaidi na ndiyo sababu sasa tumekuja na Yas badala ya Tigo ya awali,” amesema Albou.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mixx by Yas iliyojulikana kwa jina la Tigo pesa, Angelica Pesha amesema wameamua kuita Mixx by Yas kwa sababu inamgusa kila mtu kwenye jamii.

“Inamgusa mwenye elimu na asiye na elimu. Kwa jumla yeyote mwenye mahitaji ya huduma za kifedha akitumia Yas, basi inakuwa imemjumuisha katika jukwaa bora zaidi,” amesema Pesha. 

Amesema miongoni mwa mikakati yao ni kuhakikisha wanashirikiana na taasisi za kifedha nchini kwa lengo la kuwafikia watu wote wakiwamo wajasiriamali kila wanavyoboresha  huduma zao.

Hata hivyo, amesema licha ya kubadili jina, lakini huduma zao bado zinabaki kuwa zile zile.

 “Mtandao wa Yas unadhamira ya kuongoza katika ubunifu wa kidijitali na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi Tanzania nzima,”amesema Pesha.

Amesema mabadiliko hayo ni ishara ya dhamira ya kampuni hiyo kuendelea kuwekeza na kuendeleza mabadiliko ya kidijitali Tanzania Bara na visiwani kwa kuendelea kufungua fursa mpya, kuhamasisha ubunifu, kujenga kesho iliyobora na kuunganisha watu zaidi.

Pesha amesema Yas na Mixx by Yas zinadhamiria kubeba maono ya kampuni ya kuwa kiungo muhimu cha ubunifu wa kidijitali Afrika kwa kutengeneza fursa zisizo na kikomo sambamba na kuboresha maisha kupitia huduma za kidijitali na huduma za kifedha kwa mamilioni ya Watanzania.

Awali, mtandao huo ulibadili chapa ya kampuni iliyokuwa ikijulikana kama Tigo Tanzania hadi kuitwa Yas.

Tigo ambayo wakati inaingia nchini miongo mitatu iliyopita, ilianza kwa jina la Mobitel kabla ya kuitwa Tigo na ilibadilishwa jina lake hilo Novembe 26, 2024 na sasa inaitwa Yas.

Mbali na kubadilika kwa chapa ya kampuni pia jina la huduma zake za miamala ambazo awali zilijulika kama Tigo pesa nazo zimebadilika kutoka jina hilo na sasa inaitwa Mixx by yas.

Yas (zamani Tigo) inamilikiwa na kampuni ya Honora Tanzania Public Limited ambayo ni sehemu ya kampuni mama ya Axian Telecom Group.

Related Posts