Baba adaiwa kujinyonga baada ya kumchinja mtoto wake

Shinyanga. Mkazi wa Kijiji cha Mwamagunguli, Kata ya Kolandoto Manispaa ya Shinyanga mkoani humo, Peter Makoye (45) amekutwa amejinyonga kwa kutumia kamba ndani ya nyumba yake.

Tukio hilo limetokea leo Jumatatu, Desemba 2, 2024, saa 11 alfajiri, huku marehemu akidaiwa kuchukua uamuzi huo muda mfupi baada ya kudaiwa kumjeruhi mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka sita kwa kumchinja shingoni kwa kutumia kisu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kwa sharti la kutorekodiwa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amesema uchunguzi wa awali umebaini mwanaume huyo kabla ya kujinyonga alikuwa na mgogoro wa shamba na mkewe.

Kamanda Magomi amesema mwanaume huyo aliingia katika ugomvi na mkewe akimtuhumu kuuza mashamba ya familia bila kumshirikisha, jambo ambalo lilimkwaza na kumsababishia hasira za kila mara.

“Ni kweli tukio hilo limetokea katika Kata ya Kolandoto na chanzo cha mgogoro ni mwanaume ambaye ni marehemu kuuza mashamba bila kumshirikisha mkewe, ndipo ugomvi ulipoanzia,” amesema Magomi.

Mwili wa marehemu umechukuliwa na polisi kwa uchunguzi, kisha kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika HospitalI ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga (Mwawaza).

Awali, kiongozi wa sungusungu Kata ya Kolandoto, Luhende Seni amedai baada ya mwanaume huyo kujaribu kutekeleza unyama huo, mkewe Elizabeth Mwigulu alikimbilia kwa majirani kuomba msaada wa kumnusuru mtoto wake, lakini walipofika walikuta ameshafanya tukio jilo.

“Saa 11 alfajiri sungusungu tuliitwa tukapewa taarifa kwamba kuna mtu amejinyonga baada ya kumjeruhi mtoto wake kwa kumchinja na kitu chenye ncha kali. Tulipofika tukaona mwili unaning’inia ndipo tukatoa taarifa polisi,” ameeleza Seni.

Shuhuda wa tukio hilo, Aneth Paulo amesema baada ya kufika eneo hilo aliona mtoto huyo akiwa na jeraha nyuma ya shingo yake linalodhaniwa kusababishwa na kuchinjwa na kitu chenye ncha kali, alichukuliwa na kukimbizwa hospitali.

“Baada ya kusikia filimbi ya Sungusungu tukasogea eneo la tukio ndipo tukakuta amejinyonga ndani ya nyumba. Mtoto alikuwa hapo pembeni akachukuliwa na mama yake na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu,” amesema Aneth.

Jirani wa familia hiyo, Stella Ngelageza amesema baada ya kusikia yowe ikipigwa alisogea kwenye nyumba hiyo na kuelezwa Makoye amefariki kwa kujinyonga baada ya kujaribu kumchinja mtoto wake.

Related Posts