WANUFAIKA TASAF WENYE ULEMAVU WAISHUKURU TASAF KUBADILISHA MAISHA YAO, WATOA NENO KWA RAIS DK.SAMIA

Na Mwandishi Wetu

WANUFAIKA wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) hususani wenye ulemavu wa aina mbalimbali wametoa shukrani kwa Mfuko huo kwa kubadilisha maisha yao kupitia fedha za ruzuku huku wakitoa rai kuwa mfuko huo kuangalia uwezekano wa kuendelea kuwasaidia zaidi sambamba na kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kulisaidia kundi la watu wenye ulemavu.

Wametoa kauli hiyo leo Desemba 2,2024 ikiwa ni siku moja kabla ya kuadhimisha Siku ya Walemavu Duniani ambayo huadhimishwa Desemba 3 ya kila mwaka ambapo wanatumia nafasi hiyo kueleza kwa Waandishi wa habari mafanikio waliyoyapata baada ya kuingia TASAF mwaka 2014 na kuondolewa katika mfuko huo mwaka jana.

Wanufaika hao wenye ulemavu wamesema kupitia Mfuko wa TASAF wameweza kuanzisha biashara mbalimbali kama kuuza karanga, kutengeneza batiki, viungo vya chai na chakula pamoja na sabuni na kupitia biashara hizo wamekuwa wakipata fedha kujikimu kimaisha.

Mnafaika wa TASAF Amina Mrupe kwenye ulemavu wa viungo vya mwili anayeishi Mlandizi Mtongani katika Kata ya Mtongani Mkoani Pwani amesema kuwa kupitia TASAF alikuwa akipata ruzuku ya kila mwezi Sh.30,000 lakini baadae akawa anapewa Sh.12000 maana alikuwa anaishi na ndugu zake lakini kwa sasa anaishi na mumewe tu.

Ameongeza mbali ya kupewa ruzuku hiyo ya kila mwezi ambayo walikuwa wanapatiwa kila baada ya miezi miwili pia amepewa mtaji wa Sh.500,000 ambazo zimemuwezesha kuanzisha biashara ya batiki pamoja na kuuza karanga Mbichi na za kukaanga.

“TASAF nimejiunga mwaka 2014 , mwaka 2023 tuliondolewa ili kutoa nafasi kwa wengine.Kabla ya TASAF nilikuwa nafanya biashara ndogo ndogo kama kutengeneza Ubuyu, bisi ,karanga mbichi na kavu lakini baada ya ya kuingia TASAF nikaanza kupata ruzuku na sasa natengeneza batiki lakini wakati huo huo nikawa naendelea kuuza na karanga

Pamoja na kusaidiwa na TASAF ametumia nafasi hiyo kumuomba Rais Samia kuendelea kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa kuwapa ruzuku ambazo zitawasaidia kufanya shughuli za kiuchumi kujipatia riziki.

Kwa upande wake Nuru Ally mkazi wa Kata ya Kigogo jijini Dar es Salaam kwenye ulemavu wa jicho kutoona amesema wakati kesho Dunia ikiadhimisha siku ya Walemavu Duniani anaishukuru TASAF kwa kubadilisha maisha yake kwani amekuwa katika Mfuko huo tangu mwaka 2014 na aliondolewa mwaka jana na kwa sasa TASAF imekuwa ikimtembelea na kufuatilia maendeleo ya biashara zake.

Amesema kuwa kupitia TASAF ameweza kuwa anatengeneza viungo vya chai, chakula kama viungo vya pilau pamoja na sabuni ya chooni na hivyo kuendesha maisha yake huku akiomba kama kuna uwezekano basi arudishwe katika Mfuko huo ili apate ruzuku kwa ajili ya kufanikisha mipango yake.

Amesema Walemavu wamekuwa wakionekana kama wanapenda kuwa ombaomba lakini kupitia TASAF amekuwa akifanya shughuli zinazomuingizia kipato na kuweza kuhudumia familia yake akiwa na watoto wanne.

Hata hivyo wanufaika hao wamesema changamoto kubwa waliyonayo ni soko la kuuza biddhaa wanazotengeneza kwani wateja wanaponunua wanakaa muda mrefu bila kununua tena, hivyo wakiwa na soko la uhakika wanaaamini biashara zao zitawanufaisha.



Related Posts