Kanda ya Ziwa. Wakati kaya 424 za Kata ya Lamadi mkoani Simiyu na Rorya Mkoa wa Mara zikikosa makazi baada ya nyumba zao kuzingirwa na maji ya Ziwa Victoria, zaidi ya visiwa vya uvuvi 26 vimeathiriwa na maji hayo.
Kati ya kaya hizo, 413 ni kutoka vitongoji vya Lamadi, Makanisani na Itongo mkoani Simiyu na 11 zenye watu 188 ni kutoka vijiji vya Rwang’enyi na Busurwa wilayani Rorya.
Baadhi ya wakazi wake wameondoka maeneo hayo na kutafuta hifadhi kwa majirani na maeneo yaliyotengwa na Serikali huku wengine wakiendelea kuishi kwenye nyumba zao zilizojaa maji hayo.
Hali hiyo imesababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini huku Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ikitahadharisha kwamba mvua hizo zitaendelea kunyesha, hivyo wananchi wachukue hahadhari.
Hali ilivyo Lamadi, Rorya
Diwani wa Lamadi, Bija Laurent amesema wananchi wa maeneo yaliyoathiriwa na maji hayo baada ya kuongezeka Ziwa Victoria hawana chakula kwa kuwa walivyokuwa wamehifadhi ukiwamo mpunga, mahindi, mchele na unga vimelowa.
“Tunahitaji huduma za kijamii, kuna familia magodoro yamelowa, kuna familia zinahitaji mablanketi kwa sababu bado zinaishi kwenye nyumba zenye maji, kwa hiyo tunahofia watu wataugua nimonia, mlipuko wa magonjwa kama kipindupindu kwa sababu vyoo vimeshachanganyikana na maji, mbu pia wameongezeka. Tunahitaji neti kwa ajili ya watu kujisitiri,” amesema.
Amesema wanaendelea kuhamasisha watu wote kuhama maeneo hayo, akiiomba kupitia mfuko wa maafa kuangali namna ya kuwasaidia wakati wananchi wakiendelea kujipanga namna ya kupambana na hali hiyo.
Mkazi wa Itongo wilayani Busega, Ester Yohana anayeishi kwenye nyumba iliyojaa maji amesema hivi sasa kila kitu kufanya ni shida kutokana na maji hayo, kuanzia kujisaidia hadi mazingira ya kuishi.
Ester amesema hata miguu ya baadhi ya wazee kama yeye imeanza kuuma kwa ajili ya kukanyaga maji yenye mchanganyiko wa uchafu wa chooni.
“Upepo ukipiga tu maji yanakuja hadi huku, tuna maisha magumu sana kwa sababu ukiangalia maji hadi ndani tunafamilia, tuna watoto, chakula kimeshalowana, chumba cha kupanga kwa sisi wenye familia, kimoja unaambia kuanzia Sh50,000 au Sh40,000, unaambiwa ulipie miezi mitatu na uwezo hatuna, tunakosa cha kufanya, inabidi tukae hivyo hivyo kumuomba Mungu,” amesema Ester.
Inadaiwa maji hayo yalianza kusogea taratibu kwenye makazi ya wananchi hao kuanzia Aprili 25, 2024 na hadi kufikia Mei Mosi yalikuwa mengi kiasi cha kujaa nusu ya urefu wa nyumba za baadhi ya wakazi hao.
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka amesema tayari Serikali imaziagiza kaya hizo kutokurejea kwenye makazi yao ya awali kwa kuwa maeneo hayo sio salama kuishi.
Chikoka amesema waliokumbwa na hali hiyo ni watu 141 wa kaya nne katika kijiji cha Rwang’enyi na watu 47 kutoka katika kaya saba katika Kijiji cha Busurwa.
“Nyumba hizi ziko jirani sana na ziwa, hivyo sio salama kabisa ingawa kwa sasa madhara yaliyotokea ni nyumba kujaa maji kutokana na maji kuongezeka ziwani, hivyo sio vema kuwaruhusu warejee katika makazi hayo hata kama maji yakipungua.
“Tumepeleka vyandarua na dawa za kutibu maji, hivi tunavyoongea tunajiandaa kupeleka misaada ya chakula hasa kwa kaya zilizoathirika kwani hivi sasa wanawategema majirani na ndugu,” amesema Chikoka.
Kwa upande wa Musoma, mkuu wa wilaya hiyo, Dk Halfan Haule amesema kumekuwepo na ongezeko kubwa la maji ndani ya Ziwa Victoria hali inayoweza kuwa na athari kwa binadamu na viumbe hai vingine.
Amesema kutokana na hali hiyo Serikali wilayani Musoma imefanya vikao katika vijiji vilivyopo pembezoni mwa Ziwa Victoria na mabondeni na kuainisha maeneo salama yanayoweza kutumika endapo kutatatokea dharura waweze kukimbilia
Akizungumzia hali ya visiwa mkoani Mara, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo, Agostino Magere amesema hadi sasa kisiwa kilichozama ni kimoja tu cha Nyasahungu kilichopo wilayani Musoma na wavuvi wamehamishiwa katika Kisiwa cha Kagongo kuendelea na shughuli zao.
“Ni kweli kuna ongezeko kubwa sana la maji ndani ya Ziwa Victoria lakini hadi sasa ni kisiwa kimoja ndicho kimezama ingawa tunafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea katika visiwa vingine,” amesema Magere.
Katibu wa Chama cha Wavuvi Tanzania (Tafu), Jephta Machandalo amesema hadi sasa tayari kambi 26 kwenye visiwa vya uvuvi zimeathiriwa na ongezeko la maji ya Ziwa Victoria kati ya visiwa 58 vilivyopo ziwani humo.
Ameiomba Serikali ifanye tathimini ili kuwe na mipaka ya watu kuishi maeneo kama hayo, akishauri wahamie nchi kavu wakiendelea na shuguli zao wakiwa kwenye mwambao wa nchi kavu au visiwa vikubwa.
“Kulingana na taarifa ambazo nimezipata kutoka kwa wavuvi, ni maeneo mengi ambayo inasemekana kambi za wavuvi zilizojengwa karibu na mwambao wa ziwa zimeendelea kumezwa na maji.
“Kwa kukadiria visiwa kama 26 ambavyo nimepata taarifa navyo kati ya visiwa zaidi ya 58 vilivyopo Ziwa Victoria vimepata athari,”amesema Machandalo.
Taarifa ya Machandalo inathibitishwa na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Buhama, Jonathan Kuditha akisema nyumba 95 za wavuvi kwenye kambi ya uvuvi Kome Mchangani, Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza zimezingirwa maji yakitokea ziwani kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kuwaacha watu 100 bila makazi.
Kambi hiyo imo ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Shilaga unaosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), asilimia 90 ya wakazi wake wakijishughulisha na uvuvi na asilimia 10 wakifanya kazi nyingine.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga amesema ofisi yake ina taarifa ya nyumba za wavuvi kuzingirwa maji na kuwa tayari timu ya wataalamu ikiongozwa wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) imepita kufanya tathmini ya hali hiyo.
Mjasiriamali anayefanya kazi kwenye kambi hiyo, Amina John amesema vibanda vyao na makazi yao yamezingirwa na maji, hivyo kukosa mahala pa kuishi na kufanyia biashara zao akiiomba Serikali kuwapatia maeneo mengine.
Mvuvi kwenye kambi hiyo, Amos Jonathani amesema kutokana na adha hiyo hali ya uzalishaji mali imeshuka kutokana na maji kuvumia maeneo ya makazi na maeneo ya biashara.
Mhifadhi wa Misitu wilayani Sengerema, James Aloyce amesema TFS ilishauri maeneo ya makambi yaliyotengwa kama kuna sehemu kavu wavuvi wanaweza kusogea na kujibana kama hamna ni bora wakaondoka warudi kwao, maji yakipungua warudi tena.
Ongezeko la maji kwenye maziwa
Mhandisi Odemba Ododa kutoka Bonde la Ziwa Tanganyika amesema kina cha maji kwenye ziwa hilo kimeongezeka kwa mita tano kwa usawa wa bahari ambapo 2019 yalikuwa mita 772.35 nakufikia mita 777.22 kwa mwaka huu.
“Kwa miaka kadhaa kuanzia mwaka 2019 hadi leo 2024, maji yamekuwa yakipanda na mwaka huu hadi sasa hivi yamepanda kwa mita tano kutoka kwenye usawa wa bahari ambayo ni ongezeko la maji mengi kwa hii miaka ya hivi karibuni.
“Usawa wa bahari ni mita 772.35 na sasa hivi ni 777.22, maana yake kutoka usawa wa bahari imepanda. Kwenye miaka ya 2019 maji yalikuwa hayazidi hapo lakini baada ya mvua za miaka ya 2020 mpaka leo huo wastani umepanda kwenda juu,” amesema Ododa.
Amewataka wananchi na taasisi za Serikali kuzingatia taratibu za kisheria katika kufanya miradi yao ikiwamo kuzingatia zile mita 60 pamoja na kuwasiliana na ofisi za rasilimali za maji Bonde la Ziwa Tanganyika kujua takwimu halisi ya ziwa ili hata uwekezaji kama ujenzi wa bandari, wa soko, mialo na hoteli usipate athari au hasara siku za mbeleni.
“Tupate takwimu za ziwa zinasemaje ili tuweze kufanya kitu ambacho hakitokuwa na athari au hasara baadaye. Tunaomba wazingatie mita 60 kwa mujibu wa sheria kutoka ujazo mkubwa wa ziwa ulipofika wasifanye ujenzi au uendelezaji wowote kwa ajili ya usalama wa maji na usalama wa uwekezaji wao,”amesema Ododa.
Aprili 25, 2024, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Gerald Itimbula alisema wastani wa usawa wa maji katika Ziwa Victoria umeongezeka kutoka mita 1134.00 mwaka 2023 hadi mita 1134.86.
Imeandikwa na Saada Amir, Beldina Nyakeke na Daniel Makaka.