Miradi ya USAID Afya Yangu na Kizazi Hodari Kanda ya Kusini inayofadhiliwa na Shirika la Msaada la Watu Kutoka Marekani na kusimamiwa na Deloitte Consulting Limited, imeungana na shirika la WiLDAF Tanzania kwenye kuzindua maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kinjisia kwa mwaka 2024 huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni ‘Baada ya miaka 30 ya Beijing Tuungane kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo, mwakilishi kutoka Mradi wa USAID Afya Yangu Kanda ya Kusini Jacquiline Uwaya alisema kuwa jamii inayo mchango mkubwa Katika mapambano ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.
‘Kwa pamoja tunao uwezo wa kushawishi fikra za watu, kwani watu huchukua muda kufikiria kwa kina kila taarifa kuhusu vitendo vya ukatili inapotokea’, alisema Uwaya huku akiongeza kuwa tukishirikiana kwa pamoja kwa jamii, viongozi wa taasisi na serikali tunaweza kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Hata hivyo, alisema kuwa kwa sasa Tanzania imeweza kupinga hatua kubwa kwenye mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia ikilinganisha na miaka ya nyuma na hii imetokana na ushirikiana baina ya serikali na taasisi binafsi.
Kwa upande wake, Mgeni Rasmi Katika uzinduzi huo Balozi Getrude Mongela alisema kuwa jamii ikielimishwa ipasavyo kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsi itajiepusha na vitendo hivyo.
‘Vitendo hivi vya ukatili dhidi ya kijinsia vinatokea kwenye jamii ambayo sisi wote tunaishi. Tukiwekeza sana kwenye kutoa elimu na wote tukaungana pamoja, vitendo hivi vinaweza kuisha kabisa’, alisema Balozi Mongela.
Mongela aliongeza, ‘Jamii isiyo na ukatili wa kijinsia inawezakana, hata hivyo jamii inapaswa kuongeza juhudi za kupinga ukatili huo. Kila Mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake Katika kuhakikisha ukatili wa kijinsia unatokomezwa.