Mjadala ongezeko la shule za umma za Kiingereza

Haikuwa taharuki ndogo kwa wazazi wanaosomesha watoto katika Shule ya Msingi Ubungo NHC ya mkoani Dar es Salaam.

Kiini cha taharuki hiyo iliyotokea Novemba mwaka huu na kuzua mjadala mkubwa mitandaoni, ni taarifa waliyodai wazazi kuwa wameambiwa shule hiyo ya umma inabadilishwa na kuwa ya mchepuo wa Kiingereza, hivyo wawahamishe watoto wao.

Kwa Manispaa ya Ubungo ikiwa shule hiyo itajibadili na kuwa shule ya mchepuo wa Kiingereza, itaongeza orodha ya shule za aina hiyo kufikia zaidi ya tano zilizopo katika Jiji la Dar es Salaam pekee.

Ongezeko shule za umma za Kiingereza

Wakati zamani, ungeweza kuhesabu shule za aina hiyo kwa nchi nzima na zisifike hata 10, sasa hali imebadilika, ni kama kuna msukumo fulani wa Serikali kutaka kuwa na shule nyingi za aina hiyo.

Je, hiyo ni ishara kuwa Tanzania inataka kuondokana na mfumo wa elimu ya msingi unaotumia lugha ya Kiswahili? Ikiwa hivyo, nini hatima ya Kiswahili ambayo ndio lugha ya Taifa?

Kwa mujibu wa Waziri Ofisi ya Rais- Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, hadi kufikia Septemba, 2024, Serikali ilikuwa na jumla ya shule 68 za ngazi ya elimu ya msingi zinazotumia lugha ya Kiingereza.

Akifungua shule ya mchepuo hiyo ya Chifu Zulu ya mkoani Ruvuma, alisema, shule hizo zimeanzishwa kwa lengo la kusaidia watoto na wazazi wenye uhitaji wa shule hizo kwa gharama nafuu.

“Shule hii imeanzishwa kwa lengo la kuwasaidia watoto na wazazi wanaohitaji huduma ya shule bora yenye mchepuo wa Kingereza kwa gharama nafuu zaidi na pia inatoa elimu ya tehama kwa vitendo na inafundisha somo la Kifaransa ili kuendana na soko la dunia katika ajira na mawasiliano, ”alisema Mchengerwa.

Hata hivyo, kumekuwa na mitazamo tofauti kuhusu uanzishwaji wa shule hizo ikionekana uwekezaji mkubwa unafanyika kwenye shule hizo, ikilinganishwa na shule za mchepuo wa Kiswahili, hali inayosababisha wazazi wengi kuzikimbilia shule hizo.

Rahma Mohamed, mkazi wa Mtoni Kijichi na mzazi wa mwanafunzi anayesoma katika mojawapo ya shule za mchepuo wa Kiingereza jijini Dar es Salaam, anasema alipambana kuhakikisha mtoto wake anasoma katika shule hiyo kwa kile anachoamini inatoa elimu bora.

“Ningekuwa na uwezo mtoto wangu angesoma kwenye hizo shule binafsi za kulipia kwa sababu naamini sasa hivi Kiingereza ndiyo kila kitu. Tunashuhudia huku mitaani wanaojua vyema lugha hiyo hawalali njaa, niliposikia kuhusu shule ya Mivinjeni nikaona nimpeleke huko na si haba anaweza kujielezea vizuri kwa Kiingereza,” anasema Rahma.

Kwa upande wake, Malick James mkazi wa Charambe anasema amekuwa akizifuatilia shule hizo na kugundua maisha ya wanafunzi hayana tofauti na wale wanaosoma kwenye shule binafsi za kulipia.

“Kuna mtoto wa dada yangu anasoma kwenye hizo shule za Serikali za kulipia, kwa kifupi wako vizuri kuanzia kwenye masomo, mazingira shuleni na wana hadi usafiri unaowafuata nyumbani wanafunzi.Hata mwonekano wa watoto ukiwaangalia ni wasafi, wana jiamini huwezi kulinganisha na hawa wa hizi shule zetu za kawaida,” anasema James.

Mkurugenzi wa shirika la Hakielimu, Dk John Kalage anasema watu wengi wanakimbilia kwenye shule hizo, kutokana na dhana kuwa shule za umma za mchepuo wa Kiingereza, zina hadhi kuliko zile za umma zinazofundisha kwa Kiswahii.

Anasema sababu kubwa ya wazazi wanaotamani watoto wao kusoma shule za msingi zenye mchepuo wa Kiingereza, inatokana na ukweli kwamba Kiingereza hutumika kama lugha ya kufundishia na kujifunzia katika shule za sekondari na kwamba lugha hiyo haifundishwi vizuri katika shule za mchepuo wa Kiswahili.

“Wengi hawafahamu kwamba sera inazipa hadhi sawa lugha zote mbili. Ni jukumu la Serikali kuondoa dhana potofu kwa wananchi na kwa viongozi kuwa shule za msingi za umma za Kiingereza, zina hadhi zaidi ya zile za mchepuo wa Kiswahili.Pia itengeneze mazingira yenye usawa kwa shule za michepuo yote ya Kiswahili na Kiingereza.

“Tathmini tuliyofanya imeonesha kwamba shule hizi za mchepuo wa Kiingereza, zinafanyiwa uwekezaji mkubwa hali inayotengeneza mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia kuliko za mchepuo wa Kiswahili. Mazingira haya bora yamechangia wastani wa ufaulu wa shule za umma za mchepuo wa Kiingereza uwe juu kwa asilimia 98 ukilinganisha na asilimia 80 kwa shule za umma za mchepuo wa Kiswahili.

Mdau wa elimu, Ochola Wayoga anasema Serikali inapaswa kuweka mazingira ambayo yatafanya mfumo wa elimu kuwa na usawa, vinginevyo itakuwa mwanzo wa kuruhusu matabaka.

Anasema kuwa na shule za mchepuo wa Kiingereza ambazo mazingira yake ya kujifunzia yanaonekana kuwa tofauti kabisa na shule za mchepuo wa Kiswahili, hakuleti usawa.

Wayoga anasema katika shule hizo watoto wanalipa ada na michango mingine inayowawezesha kupata chakula, usafiri na huduma nyingine muhimu ambazo kila mzazi anatamani mtoto wake azipate akiwa shuleni.

“Mfumo huu hauleti ulinganifu wa utoaji elimu ulio sawa kwa watoto wote. Inawezekana mzazi akataka kumpeleka mtoto wake huko lakini kwa sababu hawezi kulipa gharama iliyowekwa ataishia kunung’unika.

“Binafsi siamini kama elimu bora ni shule kufundisha kwa Kiingereza na kama tunafikiri hivyo basi shule zote ziwe na mchepuo huo kuliko haya matabaka ambayo tumeanza kuyatengeneza”anasema Wayoga.

Wakati hao wakieleza hivyo, Mhadhiri wa chuo cha St John Shadidu Ndosa anapongeza mpango huo wa Serikali kuanzisha shule za mchepuo wa Kiingereza.

Anasema hatua hiyo inadhihirisha namna ambavyo nchi inaweza kutekeleza mipango yake pindi inapoamua hata kwa kuanza kwa udogo.

“Hili limetuonesha kwamba tukiamua kufanya uwekezaji inawezekana, tumeona tangu mpango huu uanze hauna muda mrefu, lakini halmashauri zimeweka nguvu shule kadhaa zimejengwa na tayari zimeanza kuchukua wanafunzi,”

Hata hivyo, Ndosa anatoa angalizo kwamba uanzishwaji wa shule hizo usiwe kichaka cha kushindwa kuwekeza kwenye shule za mchepuo wa Kiswahili.

Anasema: “Kwa kuwa Serikali ina wajibu wa kutoa elimu bora kwa wote, ni vyema vigezo na uwekezaji unaowekwa kwenye shule hizi, ukafanyika pia katika shule za mchepuo wa Kiswahili ambazo zinategemewa na Watanzania wengi.

Anaongeza: “Inawezekana michango na ada inayotolewa na wazazi kwenye shule hizi ndiyo inasaidia katika kuzijengea mazingira wezeshi, hiyo isiwe sababu ya kuziacha zile shule nyingine maana si wazazi wote wana uwezo wa kulipia”.

Mara kadhaa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amenukuliwa akisema mpango wa Serikali wa kuanzisha shule zake zinazofundisha Kiingereza, unalenga kuwapa wazazi machaguo wanayoweza kuyamudu katika kuamua hatima ya elimu ya watoto wao.

Katika mahojiano aliyowahi kufanya na gazeti hili kuzungumzia suala hilo, Profesa Mkenda alisema maoni ya kuanzisha shule za mchepuo wa Kiingeraza yalitoka kwenye halmshauri na sio msukumo wa Serikali kwa kuwa zina gharama.

“Tunataka kuboresha shule zote bila kujali ni English Medium au Kiswahili Medium. Matakwa ya kufanya English Medium yanatoka kwenye halmashauri na mara nyingi wakianzisha ili mzazi apeleke mtoto wake pale ni lazima atoe pesa.

“Sasa kama Serikali hatuwezi kusema tunahamasisha shule hizo kwa kuwa tunafahamu si wazazi wote wana uwezo wa kulipa. Tunachokifanya ni kuweka mazingira yatakayowezesha shule zetu zote kutoa elimu bora bila kuwa na matabaka ingawa hatuzuii hizo jitihada za halmashauri endapo watakubaliana kushirikiana na wazazi.

Related Posts