MASHABIKI wa Yanga walikuwa na wasiwasi inakuwaje timu yao inakwenda Algeria kucheza na MC Alger katika mchezo wa Ligi Kuu Bara huku ikiwa na majeruhi wengi hasa wale wa kikosi cha kwanza.
Wasiwasi huo umeibuka zaidi baada ya Novemba 30, 2024 kumshuhudia beki na nahodha wao msaidizi, Dickson Job akitolewa uwanjani dakika ya 82 akibebwa na machela kutokana na kuumia goti katika mchezo wa Ligi Kuu Bara wakati Yanga ikishinda 2-0 pale Ruangwa mkaoni Lindi. Nafasi yake ilichukuliwa na Jonas Mkude.
Job ambaye amecheza mechi zote tano za kimataifa msimu huu kuanzia hatua ya awali hadi ile ya kwanza ya makundi dhidi ya Al Hilal, ameshusha presha hiyo baada ya kusema kusema anaendelea vizuri.
“Kwa sasa naendelea vizuri kwani nilishtuka kidogo goti,” alisema Job ambaye amekuwa mhimili mkubwa wa eneo la ulinzi la Yanga.
Katika kuonyesha umuhimu wake kikosini hapo, Job amefanikiwa kucheza mechi tisa kati ya 10 za Ligi Kuu Bara ambazo Yanga imecheza msimu huu.
Wakati Job akishusha presha hiyo, nyota wanne waliorejea uwanja wa mazoezi ni Khalid Aucho, Clement Mzize, Chadrack Boka na Aziz Andambwile.
Wachezaji hao wanne walikosekana kwenye mchezo wa kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika nyumbani walipofungwa 2-0 na Al Hilal kutoka Sudan huku pia wakikosekana katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Namungo ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa wikiendi mkoani Lindi.
Daktari wa Yanga, Moses Etutu, alisema hali za wachezaji waliokuwa nje ya uwanja kwa muda sasa zimetengamaa ni suala la uamuzi wa kocha kuwatumia au kuwapa muda zaidi ili waweze kujiweka kwenye utimamu mzuri.
“Boka alikuwa na wiki mbili za kujitibia, Andabwile siku kumi wakati Aucho na Mzize baada ya kuwafanyia vipimo majeraha yao hayakuwa makubwa, walipewa muda wa kupumzika, tayari wamerudi na wameanza mazoezi. Kuhusiana na suala la kucheza kwa wachezaji hao lipo chini ya benchi la ufundi zaidi lakini kwa upande wangu nimefanya kazi kwa usahihi na wachezaji wenyewe tayari wameanza kujifua, ukimuangalia Aucho alianza mazoezi siku mbili baada ya kufanyiwa vipimo na kubaini shida yake.”
Yanga ikiwa Kundi A katika michuano hiyo, imeanza kwa kufungwa na Al Hilal.