Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetenga Sh9 bilioni kufanya ukarabati wa majengo chakavu ndani ya Mji Mkongwe kwa mwaka 2024/25.
Pamoja na kiasi hicho, Serikali ina lengo la kutafuta fedha kwa wadau ili kuwa na fedha za kutosha za kuwasaidia wananchi kuyaboresha majengo hayo.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameeleza hayo jana Desemba 2, 2024 katika maadhimisho ya Siku ya Mji Mkongwe yaliyofanyika Forodhani Unguja.
“Pamoja na hatua kubwa zilizopigwa na Mamlaka ya Mji Mkongwe, Serikali imedhamiria kuongeza nguvu zaidi katika kuboresha hali ya mji huo ambao sio tu urithi wa dunia, bali pia kioo cha nchi na kitovu cha utalii ambao ndio muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar,” amesema.
Kiongozi huyo amesema hivi sasa Serikali ipo katika hatua za kukamilisha upembuzi yakinifu wa mradi wa kupitisha chini ya ardhi miundombinu yote ya umeme, mawasiliano na maji katika mji huo ili kurejesha taswira na haiba ya majengo yake.
Pia, amesema Serikali kupitia mradi wa BIG Z wa Benki ya Dunia (WB) inakamilisha mageuzi ya miundombinu ya barabara na maeneo ya wazi kwa lengo la kuboresha hadhi ya mji huo muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar hasa katika sekta ya utalii.
Rais Mwinyi ameiagiza Mamlaka ya Mji Mkongwe kuchukua hatua ya kufunika mitaro yote iliyowazi katika mji huo ili kuweka mazingira salama kutokana na maradhi, ajali na kuimarisha muonekano wa mji huo.
Ameahidi kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuyafanyia ukarabati majengo yaliyopo ndani ya Mji Mkongwe ikijumuisha uhuishaji mkubwa wa maeneo ya wazi na maeneo ya bustani.
Ameipongeza Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale pamoja na Mamlaka ya Mji Mkongwe kwa kuongeza ubunifu na wigo katika kuadhimisha siku hiyo kwa kuwa maadhimisho hayo yanaonesha umuhimu wa mji huo kuendelea kuwepo katika urithi wa miji ya dunia.
Akizungumzia mfumo wa kimtandao, Rais Mwinyi amepongeza hatua hiyo inayosaidia kuzuia upotevu wa mapato na kuondoa urasimu, hivyo nataka mfumo huo muusimamie kuona unafanywa kazi vizuri.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga amempongeza Rais Mwinyi kwa kuwa, muanzilishi wa siku hiyo kwa kuwa uongozi wake umeleta mabadiliko chanya katika urithi wa Zanzibar hususan katika Mji Mkongwe.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe, Ali Said Bakar amesema kwa sasa mji huo umekuwa ukivutia kwa wawekezaji.
Amesema Serikali ya Oman imetoa zaidi ya Dola 25 milioni za Marekani (Sh66.250 bilioni) kujenga Jumba la Beit El Ajab ili kurudi katika hali yake. Itakumbukwa jengo hilo la aina yake lilidondoka Desemba 2020 na kuua watu wawili.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni, (Unesco), Michael Toto amesema siku hiyo ya Mji Mkongwe ni muhimu na Unesco imefarijika kushiriki katika kusherehekea kwa kuwa ni suala la kuendeleza tamaduni.
Amesema watashirikiana namna bora ya kuulinda mji huo kwa faida ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.
Mmoja wa Wakazi wa Mji Mkongwe, Ahmed Saleh Mbarouk ameipongeza Serikali kuweka njia ya kuhifadhi na kuendeleza Mji Mkongwe.